Halmashauri yapongezwa kwa jitihada za kuwezesha Vikundi vya Vijana na Wanawake.
Mkurugenzi Mtendaji, Bw Raphael J. Siumbu amepongezwa na Waheshimiwa Madiwani kwa jitihada za kuwezesha Vikundi kwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani. kwa. Hayo yamesemwa kwenye mkutano wa baraza la madiwani uliofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri mnamo tarehe 24/03/2017.
‘kwa kweli Mkurugenzi amejitahidi kusimamia agizo la serikali , tumeona mabadiliko makubwa mara tu alipoanza kazi kwani miaka ya nyuma wanawake na vijana walikuwa hawapewi fursa ya kuwezeshwa kwani fedha zilikuwa hazitolewi zote’ alisema mmoja wa madiwani alipohojiwa. Alipongeza serikali ya awamu ya tano kwa jitihada zake za kuhakikisha wanawake na vijana wanashiriki katika kukuza uchumi wa viwanda.
Jumla ya vikundi 22 vya wanawake na vijana vimewezeshwa kiasi cha Tsh 66,000,000/= kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017. Mkurugenzi huyo ameahidi kuendelea kutekeleza agizo la serikali kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa fursa zaidi kwa ajili ya kuwafikia wananchi wengi zaidi kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii.
Aidha Afisa Maendeleo ya Jamii, Bw Tomas Nade ambae ni Mratibu wa Mikopo na Afisa Vijana ametoa rai kwa wanufaika wa mikopo hiyo kufanya kazi kwa bidii na maarifa na kuhakikisha wanafuata taratibu za marejesho ya fedha hizo ili vikundi vingine vinufaike na fursa hiyo ya mikopo yenye riba nafuu inayotolewa na Halmashauri.
Wakati huo huo, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Bi Teresia A Irafay ameahidi kuendelea kubuni mifumo mbalimbali ya uwezeshaji vikundi na kusimamia kwa karibu mifumo hiyo ya kuwezesha wananchi kupitia Vikundi mbalimbali vya COCOBA na VICOBA pia kusimamia utoaji wa elimu ya ujasiriamali kupitia wataalamu wake na kushirikiana na Idara zote za Halmashauri, Mashirika ya Umma, Wawekezaji pamoja na Mashirika yasiyo ya Serikali katika kuhakiksha vijana na wanawake wanapata fursa za uwezeshaji wenye tija. Aidha amesisitiza wananchi wajiunge kwenye vikundi kwa hiari yao, wabuni miradi yao, wasajili vikundi kupitia ofisi yake ili waweze kutambulika rasmi hatimae kurasimisha shughuli zao.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.