Baraza la Wafanyakazi la Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro limejadili na kupitia mapendekezo ya Bajeti ya Mapato na Matumizi, ambayo ni jumla ya shilingi bilioni 41.280,018,526.00 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Wilaya ya Ngorongoro Mkoa wa Arusha.
Baraza la Wafanyakazi limekaa kujadili bajeti hiyo leo tarehe 10 Februari 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ambapo Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii Bw. Benezeth Bwikizo ameeleza kwamba ni halali kwa kila mfanyakazi kutimiza wajibu wake na kusisitiza ushirikiano ili kuhakikisha wanafikia adhima na malengo yaliyowekwa na kuwaomba Watumishi waendelee kutekeleza majukumu kwa kuzingatia Bajeti iliyopitishwa.
Bw. Bwikizo amefafanua na kueleza kuwa kikao hicho ni maalum kwa ajili ya kupitia, kujadili na kufanya tathmini ya utendaji kazi ambapo kila mfanyakazi ana haki katika utekelezaji wa majukumu na stahiki anapowajibika kutimiza malengo yaliyopangwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Awali akiwasilisha rasimu ya Bajeti ya mwaka 2025/2026 Afisa Mipango wa Halmashauri Bi. Emmy Hongoli kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro amefafanua kwamba katika rasimu hiyo ya Bajeti kiasi cha shilingi 3,797,811,070 ni fedha zitokanazo na vyanzo vya Mapato ya ndani ya Halmashauri, kiasi cha shilingi bilioni 18,114,572,000 ni fedha ya mishahara ya Watumishi, na kiasi cha shilingi bilioni 1,092,093,000 ikiwa ni ruzuku ya uendeshaji (OC) na kiasi cha shilingi bilioni 18,275,542,456.00 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na fedha zote ni kutoka Serikali kuu na wahisani.
Aidha Bi. Emmy Hongoli ameeleza kuwa pamoja na kuwepo kwa rasimu ya bajeti hiyo ofisi ya Mipango na Uratibu imeahidi kutekeleza na kufanyia kazi mapendekezo na maadhimio ya kikao hicho ikiwa ni pamoja na kuendeleza ushirikiano ili kuhakikisha kuwa na maendeleo chanya katika jamii ndani ya Halmashauri ya Ngorongoro
Hata hivyo kupitia kikao hicho wajumbe walipata wasaa wa kupitia na kujadili pamoja na kutoa maoni yao juu ya mapendekezo ya bajeti hiyo na kupongeza namna ulivyoandaliwa .
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.