. _Rc Makalla apokelewa kwa shangwe, akifanya ziara yake Wilayani Ngorongoro
. Wananchi wamshukuru Rais Samia kwa miradi mingi ya maendeleo_
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla amefanya ziara ya Kikazi Wilayani Ngorongoro leo Jumanne Septemba 02, 2025, akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kwa kutoa zaidi ya Bilioni 88 kwaajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo Wilayani humo, ikiwemo Bilioni 18.9 zinazotekeleza miradi 17 ya Maji kwenye Kata mbalimbali za Ngorongoro.
Mhe. Makalla ameyaeleza hayo mara baada ya kupokelewa Wilayani Ngorongoro na kuzungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, akimpongeza pia Mkuu wa Wilaya hiyo Brigedia Jenerali Wilson Christian Sakulo kwa kuongeza makusanyo kwenye sekta ya mifugo kutoka Shilingi Milioni 13 kwa mwaka hadi zaidi ya Milioni 200 na kusema fedha hizo zitasaidia kuongeza uwezo wa Halmashauri hiyo katika kuwahudumia wananchi.
"Wilaya ya Ngorongoro inapokea fedha nyingi, miradi mingi mfano ukichukulia tu sekta ya maji, Wilaya hii ya Ngorongoro ina miradi 17 ya maji inayotekelezwa kwa wakati mmoja na katika miradi hiyo ya Maji Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta fedha bilioni 18.9 kutekeleza miradi hiyo na Sale yenyewe ina mradi wa maji" amesema Mhe. Makalla.
Aidha katika salamu zake, Mkuu wa Mkoa mbali ya kuhimiza kushirikiana pamoja katika kuwaletea wananchi maendeleo na kutimiza maono ya Rais Samia katika kuwatumikia wananchi, amesisitiza umuhimu wa Viongozi wa Wilaya hiyo kuendelea kulinda na kudumisha amani na utulivu katika kipindi hiki cha uchaguzi Mkuu ili kuruhusu wananchi kushiriki kikamilifu kwenye kampeni na uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Awali katika maelezo yake, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro ameeleza pia kuwa hali ya ulinzi na usalama katika Wilaya hiyo ni shwari na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo unaendelea vyema, akieleza pia kuhusu uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ambapo kwa mwaka 2024/25, Jumla ya shilingi Milioni 634 zimetolewa kwa vikundi 130 vya wanawake, Vijana na wenye ulemavu.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.