Naibu Waziri, @ortamisemitz
Mhe. Zainab Katimba amewaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana katika shule zote za Msingi na Sekondari kwenye maeneo yao.
Mhe. Katimba ametoa maelekezo hayo bungeni jijini Dododma kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti maalum, Mhe. Mwantumu Zodo, ambaye ametaka Ofisi ya Rais - TAMISEMI kushirikiana na Wizara ya Maji kuhakikisha shule hasa za kutwa zinapata maji safi na salama.
Akijibu swali hilo, Mhe. Katimba amesema “Dhamira ya serikali ni kuhakikisha katika shule zetu za msingi na sekondari huduma muhimu ya maji safi na salama inapatikana na kwa msingi iliowekwa wa ugatuzi wa madaraka kutoka serikali kuu kwenda kwenye mamlaka zetu za serikali za mitaa,Halmashauri zinawajibu wa msingi wa kuhakikisha katika shuke zetu za msingi maji safi na salama yanapatikana.”
Awali, katika swali la msingi, Mbunge huyo ametaka kujua lini Serikali itaweka mkakati madhubuti wa upatikanaji wa maji ya uhakika kwenye shule za Msingi na Sekondari nchini.
Mhe. Katimba amesema Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali kuhakikisha upatikanaji wa maji ya uhakika kwenye shule za msingi na sekondari nchini ikiwa ni pamoja na kutoa fedha kwa baadhi ya shule kwa ajili ya kuchimba visima virefu na vifupi, kujenga miundombinu ya kuvunia maji ya mvua na kununua matanki makubwa kwa ajili ya kuhifadhia maji na kutoa elimu ya namna ya kuhifadhi vyanzo vya maji vilivyopo katika maeneo yao ili maji hayo yatumiwe na shule zilizopo jirani na vyanzo hivyo.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.