Ikiwa ni katika kuboresha hali ya lishe ili kutokomeza udumavu kwa Watoto, leo tarehe 08 Februari 2024 Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro imefanya Kikao cha tathimini ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha robo ya pili ya Mwezi Oktoba hadi Disemba 2023
Kikao hicho kimehudhuriwa na Bw. Hamza Hamza, Katibu Tawala Wilaya ya Ngorongoro kama mwenyekiti wa kikao kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bw. Nassoro Shemzigwa pamoja na Wajumbe wengine wa Kikao hicho
Katika kikao hicho Bw. Hamza amewataka Watendaji wa vijiji, Kata, Katibu tarafa kushirikiana na Maafisa lishe ili kusaidia katika uboreshaji na kuimarisha hali ya lishe ndani ya Wilaya
Bw. Hamza amesema "lengo ni kufanya vizuri kwenye suala zima la lishe hivyo inabidi tushirikiane ili tuweze kuwa katika hali nzuri ya kiafya na kulinda afya za Watoto wetu ili kuepuka udumavu"
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Bw. Nassoro Shemzigwa amesema kuwa ili tuweze kuwa na tathimini nzuri ni muhimu kutengeneza utaratibu wa kujipima wenyewe.
" Lazima tujiwekee malengo kwa kila kipindi ili tuweze kujipima wenyewe mbali na mifumo iliyowekwa ili tuweze kufanya vizuri kwenye mifumo na katika kipimo chetu wenyewe" amesema Shemzigwa.
Hata hivyo Afisa lishe Wilaya Bi. Mariamu amewasilisha taarifa ya tathimini kuanzia mwezi Oktoba hadi Disemba 2023 iliyoonesha ziara za usimamizi shirikishi zimefanyika katika vituo 38 vinavyotoa huduma za mama na mtoto ili kusambaza Vitamin A, pamoja na ufuatiliaji wa Ubora wa huduma za lishe, jumla ya Watoto 42,172 chini ya miaka mitano walipatiwa matone ya Vitamin A
Aidha taarifa imeonyesha Shule 94 zilizopo Wilaya ya Ngorongoro zinatoa chakula walau mlo mmoja kwa siku, pia upimaji na utoaji wa elimu ya lishe kwa Wanafunzi umefanyika katika Shule 21 zilizotembelewa zenye jumla ya Wanafunzi 1,134 kuanzia darasa la awali na darasa la saba wamefanyiwa uchunguzi wa hali ya lishe ambapo Wanafunzi 1,127 sawa asilimia 99 wanahali nzuri huku Watoto saba sawa na asilimia 0.6 walikua na hali mbaya ya lishe na juhudi zilifanyika kuwahudumia Watoto hao pamoja na elimu ya lishe bora ilitolewa ili kuepuka matatizo yatokayo na lishe.
"Upimaji wa afya, elimu kwa vitendo ya upikaji na utumiaji wa vyakula vya nyongeza inatolewa kwa akinamama wajawazito" amesema Afisa lishe
Ikumbukwe Serikali ya awamu ya sita imeipa kipaumbele sekta ya afya na upande wa lishe ili kuboresha, kuimarisha afya za Watoto na kuondoa hali ya udumavu kwa Watoto kwa lengo la kuwa na kizazi bora na chenye afya timamu.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.