Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Kanali Wilson Sakulo leo tarehe 26 Aprili, 2024 ameongoza zoezi la upandaji miti eneo la Zahanati ya Yasimdito ikiwa ni sehemu ya kusherehekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibari.
Wadau mbalimbali wameshiriki katika zoezi la upandaji miti wakiwemo Wakuu wa Divisheni na Vitengo Halmashauri ya Wilaya, T.F.S, Shirika la F.Z.S na jamii wa Kata ya Samunge wakiongozwa na Diwani Mhe. Kajurus, Kupitia Maadhimisho hayo jumla ya Miche ya miti 2,636 imepandwa katika eneo la Zahanati ya Yasimdito.
Wakati wa kutoa taarifa fupi ya zoezi la upandaji miti kwa Mhe. Mkuu wa Wilaya, Afisa Maliasili Wilaya Bw. Nganana Mothi ameeleza kuwa lengo kuu la upandaji Miti katika eneo la Zahanati ya Yasimdito na maeneo mengine ya Wilaya ni kuboresha utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji, kukabiliana na mmomonyoko wa udongo sambamba na madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabia ya nchi na hali ya hewa.
Aidha, Kanali Wilson Sakulo ametoa pongezi kwa wadau pamoja na Wataalamu wote waliojitokeza kushiriki zoezi hilo kama sehemu ya kusherehekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kanali Sakulo aliwasihi washiriki wote kuishi na kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024 unaosema "TUNZA MAZINGIRA NA SHIRIKI UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA KWA UJENZI WA TAIFA ENDELEVU"
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.