Shirika la Frankfurt Zoological Society kwa kushirikiana na TANAPA wamekabidhi vyumba 3 vya madarasa na Madawati 40 venye thamani ya Shilingi milioni 178 kwa Shule ya Msingi ya Soitsambu iliyopo kata ya Soitsambu wilayani Ngorongoro.

Mradi huo uliofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) ni sehemu ya miradi 36 ya Afya, Elimu na Miundombinu ya ujirani mwema inayotekelezwa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika wilaya hiyo.
Akipokea Madarasa hayo Yannick Ndoinyo Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro amesema eneo lao limeshuhudia miradi mingi inayotokana na matunda ya uhifadhi na kuwaomba wazazi kuchangamkia fursa ya elimu kwa watoto wao.

“Niwashukuru FZS, TANAPA na KFW mlichokifanya ni kikubwa hii ni hatua kubwa, naomba tuelekeze nguvu katika kuwainua wananchi kiuchumi ili waweze kumudu gharama za maisha zitazowasaidia kuwafadhili watoto wao mahitaji ya msingi ya kila siku ikiwemo yale ya kielimu”.
Mbunge Yannick amewahimiza wananchi wa eneo hilo kudumisha uhifadhi kama mila yao inavyotaka kwa kuwa faida zake ni kubwa na zinaonekana kwa macho.
Masegeri Rurai Meneja Miradi wa FZS amesema “gharama za mradi huu zimekuwa kubwa kutokana na aina ya ujenzi tuliotumia kwa kuzingataia usalama kwa kuwa eneo hili linakumbwa na tetemeko la ardhi kwa sababu lipo karibu na bonde la ufa” amesema Rurai.
Mhifadhi Elisamehe Ayubu akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti amesema “tutaendelea kutekeleza miradi inayolenga kukuza taifa la kesho ndio maana unaona elimu tunaitilia mkazo, tutaendelea kushirikiana kwa namna yoyote”.
Yukabert Samwel Mwanafunzi wa Darasa la Saba amesema “tumekuwa tukitumia madarasa yasio na mwanga wa kutosha ila haya ya sasa ni mazuri yanavutia, nawashukuru waliotoa”.
Lydia Marko Mkazi wa Kijiji cha Soitsambu amesema “madarasa haya yametusaidia kupunguza gharama za michango na kupunguza msongamano kwa wanafunzi, tumefurahi na kushukuru sana”.

Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.