Kikao cha tathmini ya shughuli za utekelezaji wa lishe kipindi cha robo ya kwanza ya Julai hadi Septemba 2024 kimedhihirisha kuwa jumla ya watoto 30,940 walikutwa na hali nzuri ya lishe ambayo ni sawa na asilimia 92.81 baada ya kufanyiwa tathmini ya lishe.
Kikao hicho kimefanyika leo tarehe 19 Desemba 2024 katika ukumbi wa Mkutano wa Halmashauri na kimeongozwa na mwakilishi wa mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Ndg. Boniface Lugola ambaye ni Afisa Tawala Wilaya.
Hali ya lishe kwa Watoto imeendelea kuimarika kutokana na kuongezeka kwa asilimia za hali nzuri ya lishe. Mwenyekiti wa kikao hicho amewapongeza Wataalamu wa lishe na wadau wa afya kwa kazi nzuri waliofanya kudumisha hali nzuri ya afya na lishe kwa watoto.
"Tunawapongeza sana Maafisa lishe, Watendaji wa kata na Wataalamu wengine kwa kweli mmefanya kazi kubwa, hivyo tuendelee kufanya kazi ili kuitokomeza kabisa hali mbaya ya lishe kwa watoto wilayani kwetu".amesema Ndg. Lugola
Afisa lishe Bi. Angela Mbaga wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba 2024, amesema jumla ya Watoto 33,337 walifanyiwa tathmini ya hali ya lishe huku idadi ya Watoto 30,940 sawa na asilimia 92.81 walikutwa na hali nzuri ya lishe na asilimia 6.95 sawa na watoto 2, 317 walikutwa na hali mbaya ya lishe.
Bi.Angela Mbaga ameendelea kueleza kwa kipindi chote cha miezi mitatu walifanya maadhimisho ya siku ya afya na lishe katika kata saba (7) kati ya kata 28, kata zilizofanyiwa maadhimisho ni kata ya Maalon, Ololosokwan, Oloipiri, Kirangi, Orgosorock, Enguserosambu na Olorien Magaiduru, maadhimisho hayo yalihusisha utoaji wa huduma za kliniki ya MKOBA, upimaji wa hali ya lishe kwa watu wazima na kutoa ushauri na nasaha kuhusu lishe bora kulingana na hali za lishe.
Sanjari na hilo jumla ya akina mama 12,156 kati ya 12,511 walipatiwa vidonge vya madini chuma ili kuboresha hali ya afya kwa wajawazito, pia elimu ya lishe ya makundi ya chakula, uandaaji wa mlo kamili na chakula cha nyongeza kwa watoto wadogo ziliendelea kutolewa.
Aidha, mwakilishi wa mkuu wa Wilaya ametoa rai kwa Wajumbe wa afya kuendelea kusimamia vyema shughuli za lishe katika jamii kuanzia shuleni, nyumbani na kuhimiza miti ya matunda kuanza kupandwa mashuleni kama sehemu ya kampeni ya ulaji wa matunda kwa watoto na watu wazima katika jamii.
"Licha yakuwa tuna viashiria vizuri vya hali ya lishe, naomba tulichukue hili kama azimio sisi kama wajumbe tuhakikishe miti ya matunda inapandwa katika shule zetu, rai yangu siku ya maadhimisho ya huru wa Tanzania bara tulipanda miti ya matunda shule ya msingi Wasso hivyo rai yangu tukapande miti ya matunda ya kutosha katika shule zetu".- Ndg. Boniface Lugola.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.