Divisheni ya Afya kupitia Kitengo cha Lishe Wilaya ya Ngorongoro imeaswa kuwafuatilia kwa karibu watoto waliobainika kuwa na utapiamlo mkali, kwa lengo la kuondoa hali ya udumavu na kuimarisha lishe bora miongoni mwa watoto hao, huku jamii ikihimizwa kutoa ushirikiano katika juhudi hizo.

Rai hiyo imetolewa leo tarehe 10 Februari, 2026 na Afisa Tawala wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Boniphace Lugola, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya, wakati wa kikao cha tathmini ya lishe ngazi ya wilaya kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya.

Bw. Lugola amesema kuwa licha ya idadi ya watoto wenye utapiamlo mkali kuonekana kuwa ndogo, bado kunahitajika juhudi za pamoja katika kuwabaini, kuwatibu na kufuatilia maendeleo yao hadi hali zao za afya zitakapokuwa imara.

Aidha, Bw. Lugola amesisitiza kuwa jamii isiyo na udumavu ndiyo msingi wa maendeleo endelevu, akipongeza Divisheni ya Afya chini ya Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) pamoja na timu ya lishe kwa kuendelea kufanya ukaguzi wa vyakula, upimaji wa afya kwa wahudumu wa vyakula migahawani na hotelini, pamoja na kuimarisha usafi wa mazingira.
Akiwasilisha taarifa ya tathmini ya lishe, Afisa Lishe wa Wilaya, Bi. Angela Mbanga, amesema kuwa kitengo hicho kimeendelea kutoa huduma za matibabu kwa watoto wenye utapiamlo mkali katika Hospitali ya Wilaya, Hospitali ya Wasso na Endulen.

"kati ya watoto 64,084 waliotarajiwa kufanyiwa tathmini ya lishe, watoto 59,774 sawa na asilimia 93.27 walipimwa hali ya lishe kwa kuangalia uwiano wa uzito kwa umri. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watoto 58,628 sawa na asilimia 98.08 walibainika kuwa na hali nzuri ya lishe, watoto 1,078 sawa na asilimia 1.8 walikuwa na hali hafifu ya lishe, huku watoto 68 sawa na asilimia 0.11 wakibainika kuwa na hali mbaya ya lishe"-Bi. Anjela
Wajumbe wa kikao hicho wakiwemo viongozi wa dini na maafisa watendaji wa kata, wamepongeza juhudi zinazofanyika na kuhimiza kuendelea kutolewa kwa elimu ya lishe bora kwa jamii, ikiwemo ulaji wa mlo kamili, upandaji wa miti ya matunda na uanzishwaji wa bustani za mbogamboga shuleni.

https://www.instagram.com/p/DUlLMJWCtU0/?img_index=6&igsh=MWMycGd4aTdrYXN3
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.