Ngorongoro-Arusha
Wadau wa Maendeleo Shirika la Umoja wa mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO na FAWE Tz kupitia ufadhili wa shirika la Maendeleo la Korea ya kusini (KOICA – Korea International Cooperation Agency ) wametoa Mafunzo ya Malezi na unasihi katika shule ya Sekondari Digodigo iliopo Tarafa ya Sale wilayani Ngorongoro.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamewahusisha Maafisa Elimu Kata, wakuu wa shule za msingi na sekondari na Walimu wa Malezi na Nasihi mashuleni yenye lengo la kuwajengea uwezo walimu ili kuboresha mifumo ya kunasihi na malezi kwa wanafunzi mashuleni hasa wasichana .
Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, mkufunzi kutoka FAWE Bw; Buheri Richard Thomas Amesema mafunzo haya yatawasaidia washiriki kupata elimu zaidi kuhusu malezi na unasihi na kuongeza ufahamu juu ya mbinu anuai za kulea watoto na kutatua changamoto zinazowakabili.
Mgeni rasmi katika mafunzo haya Bw; Emanuel Mhundo akimwakilisha Katibu Tawala Mkoa amewataka washiriki kuonyesha ushirikiano kwa wakufunzi ili kuweza kufikia malengo ya pamoja ikiwa ni kupunguza utoro kwa wanafunzi pamoja na mimba kwa wanafunzi.
Hata hivyo Bw Mhundo amewashukuru wadau wa maendeleo na wawezeshaji Shirika la UNESCO na FAWE Tz kupitia ufadhili wa shirika la maendeleo la Korea ya Kusini (KOICA – Korea International Cooperation Agency ) kwa kushirikiana na serikali katika kutoa elimu kwa maafisa elimu Kata ambao ndio walezi wakuu wa wanafunzi wawapo mashuleni.
Bwana Muhundo amewataka washiriki hao kuweka mikakati thabiti ili kutokomeza mimba na vitendo vya kikatili kwa watoto wa kike ikiwemo kuwa na orodha ya wanafunzi waliopatiwa huduma ya malezi na unasihi, Maafisa Elimu kutekeleza maagizo ya serikali ya kuwachukulia hatua watuhumiwa wa mimba kwa wanafunzi ,kuwa na chumba maalum kwa ajili ya kutolea unasihi shuleni na pia kuwashirikisha wazazi au walezi pamoja na jamii juu ya mahitaji na malezi bora kwa watoto.
Kwa upande wa Washiriki Bw.Fabian Keha amesema mafunzo haya ni chachu ya kuongeza jitihada na mbinu mbalimbali za kutoa malezi bora kwa watoto mashuleni hasa wasichana ambao mara nyingi ni waoga kuwashirikisha wazazi au walezi kuhusu mahitaji na changamoto wanazokumbana nazo kutokana na mila na desturi zisizo rafiki.
Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Maelezo
Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.