Idara ya ujenzi na zimamoto ni moja kati ya Idara 13 zinazoongoza Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, ina vitengo vinne ambavyo ni Kitengo cha Usimamizi wa Barabara, Kitengo cha Usimamizi wa Majengo, kitengo cha Ufundi na Zimamoto
Kitengo cha Usimamizi wa Barabara
Wilaya ya Ngorongoro ina jumla ya kilometa 806 za mtandao wa barabara. Kati yake Kilometa 492.1 ni za moramu na 313.9 ni za udongo 55.7 % ni barabara ambazo zinapitika bila changamoto kubwa, zipo kwenye hali nzuri, 18.6 % ni barabara zinazoridhisha kupitika na 41.4 % zipo katika hali mbaya, barabara zinazohitaji matengenezo makubwa. Wakati wa Msimu wa mvua takribani 60% ya barabara kuu ya wilaya na barabara zinazounganisha vijiji na vijiji zinapitika kwa tabu hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya jamii. Idara kupitia Bajeti ya mfuko wa Barabara inaendelea kutekeleza majukumu yake.
Kitengo cha Usimamizi wa Majengo
Kitengo hiki kinasimamia ubunifu na ujenzi wa majengo ya serikali, na taasisi za serikali pamoja na taasisi za jamii pamoja na ya wananchi. Pamoja na usimamizi huo, bado jamii haijatambua Umuhimu wa kuwatumia wahandisi wa Majengo katika kusimamia majengo yao na kutoa ushauri wa kitaalamu kabla ya ujenzi na wakati wa ujenzi. Hivyo Idara inatoa rai katika kutumia Wahandisi wa Halmashauri.
Kitengo cha Ufundi.
Kitengo hiki kinahusika kuratibu karakana ya Halmashauri ikiwa ni pamoja na kutunza na kufanya matengenezo ya magari ya halmashauri na vifaa vyote vya usafiri vya Halmshauri. Pia kitengo kinahusika kuratibu utengenezwaji wa magari na vifaa vingine vya usafiri kwenye karakana ya TEMESA na karakana Binafsi.
Aina zingine za Usafiri na Mawasiliano ya Simu yaliyopo.
Wilaya ya Ina jumla ya viwanja vidogo vya Ndege 15 ambavyo vinawezesha watalii kufika kwa haraka maendeo ya Utalii, na pia vinatumika kwenye uwezeshaji wa Madaktari na Wahudumu wa Afya kufika maeneo yasiyofikika kwa urahisi kwa ajili ya kutoa huduma za afya kama vile chanjo. Wilaya ina uwanja wa ndege mdogo mmoja tu ambao unapokea ndege kubwa. Uwanja unaomilikiwa na Kampuni ya Uwindaji ya OBC . Viwanja vingine vina uwezo wa kupokea ndege ndogo tu.
Huduma za mitandao ya Simu:
Huduma hii wilayani Ngorongoro hutolewa na makampuni binafsi na shirika la Umma. Mpaka sasa Wilaya inahudumiwa na Makampuni manne ya simu ambayo ni Kampuni za Tigo, Airtel, Vodacom na Zantel. Aidha TTCL inahudumia Wilaya kwa mfumo wa mawasiliano ya Simu ya Mezani. Kwa maeneo machache ambayo yanakabiliwa na changamoto ya mawasiliano ya simu, Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo imefunga mfumo wa redio upepo kwenye kata na vijiji
Huduma ya Radio na Televisheni/Luninga
Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro mpaka sasa haina kituo cha redio na Televisheni. Huduma hii inapatikana pale tu mwananchi atakapokuwa na kingamuzi. Aidha wananchi wengine hupata huduma hii nchi jirani ya Kenya ambapo husikiliza vituo vya radio na TV za Kenya.
Huduma za Umeme
Wilaya ya Ngorongoro ni moja kati ya wilaya zinazopata huduma za umeme kwenye makao yake makuu. Umeme unaotolewa kwa njia ya jenereta, na wahudumu/wasambazaji wakuu ni Shirika la Umeme Tanzania, TANESCO. Kati ya tarafa tatu zinazounda wilaya ya Ngorongoro, ni Tarafa moja tu inayopata huduma ya Umeme kutoka TANESCO, Mji wa Wasso- Loliondo ndio unapata huduma hiyo. Baadhi ya Vijiji vingine vinapata huduma ya nishati ya umeme kutoka kwenye makampuni binafsi kama M POWER.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.