Kitengo cha sheria ni moja vitengo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Kitengo hiki kinaratibu masuala yote yanayohusu Sheria mbalimbali, kinatoa ushauri wa kitaalamu kwa Mkurugenzi Mtendaji, kwenye vikao vya kisheria vya Halmashauri, na pia kutoa ushauri wa kisheria kwa mamlaka za vijiji ama mtu mmoja mmoja au vikundi kwenye vijiji na kata zinazounda Halmashauri.
Kwa miaka mitano iliyopita, kitengo hiki kiliandaa na kusambaza kabrasha la mfano wa mikataba mbalimbali ambayo vijiji vinatakiwa kutumia katika kuingia mikataba na wawekezaji ama wahisani mbalimbali kwenye vijiji ambapo vijiji vyote 72 vilipata Kabrasha hili la mfano.
Aidha, Kitengo kinatoa mafunzo ya namna ya kuandaa sheria ndogo za vijiji, kinajenga uwezo kwa wajumbe wa mabaraza ya ardhi na kusimamia kesi mbalimbali za Halmashauri.
Pamoja na majukumu hayo, wananchi bado wanakabiliana na changamoto ya kutofahamu sheria za nchi, na sheria ndogo, vijiji kuingia mikataba na wadau bila kufahamu kwa kina aina ya mkataba na hatimae kupata madhara baadae. Kitengo kwa kuona changamoto hiyo, kinaendelea kujenga uwezo kwa viongozi wa vijiji na wa halmashauri kupitia vikao mbalimbali na makongamano.