Halmashauri saba za mkoa wa Arusha zimekutana kujadili tathmini ya utekelezaji wa mpango wa bajeti na ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026. Kikao hicho kimeangazia mbinu za kuongeza mapato na kuhakikisha matumizi ya bajeti yanaendana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo husika.
Katika kikao hicho, wataalamu wa halmashauri walikubaliana kutekeleza miradi ya maendeleo kwa uadilifu kulingana na bajeti inayotolewa na Serikali. Pia walisisitiza umuhimu wa kulipa madeni ya watumishi na wazabuni kwa wakati, kuacha tabia ya kulimbikiza madeni, na kusimamia matumizi bora ya fedha za umma.
Washiriki wa kikao hicho walijadili pia njia bora za kupunguza hoja za ukaguzi na kuziondoa kabisa, huku wakizipongeza halmashauri zilizofanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha. Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro imeongoza kwa kufikisha asilimia 28 ya makusanyo ya mapato ya ndani, ikifuatiwa na Halmashauri ya Karatu.
Mgeni rasmi katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bw. Bennezeth Bwikizo, alitoa pongezi kwa wajumbe wote kwa kuendesha kikao hicho kwa mafanikio na kupongeza uamuzi wa kufanya vikao hivi kila robo ya mwaka ili kuchochea uboreshaji wa utendaji kazi. Kikao hicho kilihudhuriwa na maafisa maendeleo ya jamii, maafisa ugavi, maafisa utumishi, wahasibu na wakaguzi wa ndani kutoka halmashauri zote za mkoa wa Arusha, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kuboresha utendaji kazi.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.