Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mhe. Brigedia Jenerali Wilson Sakulo, mnamo tarehe 8 Januari, 2026 aliongoza Kamati ya Usalama ya Wilaya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Bw. Murtallah S. Mbillu, kutembelea familia ya mkazi wa eneo la Samunge aliyepotea baada ya kudhaniwa kuzama katika maji.

Ziara hiyo imelenga kutoa pole na kuwapa faraja wanafamilia wa mhanga huyo, ambaye ameendelea kupotea kwa siku kadhaa huku juhudi za kumtafuta zikiendelea kufanywa na vyombo vya usalama.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Sakulo amesema Serikali ya Wilaya ya Ngorongoro itaendelea kuwa bega kwa bega na familia hiyo katika kipindi hiki kigumu, huku Jeshi la Polisi likiendelea na oparesheni ya utafutaji hadi mhanga huyo atakapopatikana.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ameeleza kuwa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri itashughulikia mahitaji muhimu ya shule kwa watoto wa familia hiyo, yakiwemo madaftari, kalamu na sare za shule, ili kuhakikisha watoto hao hawaathiriki kielimu kutokana na tukio hilo.

Katika hatua nyingine ya kuwafariji na kusaidia familia hiyo, Mhe. Sakulo alikabidhi kiasi cha shilingi laki mbili za kitanzania(Sh 200,000) kama sehemu ya mchango wa Serikali wa kusaidia juhudi za utafutaji wa mpendwa wao.

Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.