Walimu wakuu wa shule za sekondari na msingi pamoja na Maafisa Elimu Kata wilayani Ngorongoro wamepatiwa mafunzo ya Mfumo wa Taarifa za Shule (SIS) unaoratibu usajili wa wanafunzi na walimu pamoja na ufuatiliaji wa maendeleo ya kitaaluma, mienendo ya tabia za walimu, pamoja motisha ya kitaaluma shuleni.

Akifungua mafunzo hayo leo Januari 07, 2026, Afisa Utumishi wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Emmanuel Mhando, akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, amewataka walimu hao kutumia mfumo wa SIS kama nyenzo ya kuboresha maendeleo ya taaluma katika shule zao.

Bw. Mhando amesisitiza walimu wakuu kuhakikisha wanatumia mafunzo hayo kuwajengea uwezo walimu wengine, pamoja na kuwasajili walimu wote wakiwemo wa ajira za kudumu, mkataba na wale wanaojitolea katika mfumo wa SIS.

Aidha, amewataka Maafisa Elimu Kata kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mfumo wa SIS kama sehemu ya majukumu yao ya utendaji kazi ili kuhakikisha matumizi sahihi ya mfumo huo katika shule zote.
“Maafisa Elimu endeleeni kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Mfumo wa Taarifa za Shule (SIS) kama sehemu ya utendaji kazi wenu,” amesema Bw. Mhando.

Akihitimisha hotuba yake, Bw. Mhando amewaelekeza walimu wakuu kuhakikisha wanafunzi na walimu wote wamesajiliwa katika mfumo wa SIS, kuandaa mpango kazi wa usimamizi wa mifumo, pamoja na kusimamia mafunzo endelevu kwa walimu.

Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, yakilenga kuboresha ufuatiliaji wa maendeleo ya kitaaluma na mahudhurio ya wanafunzi kwa kipindi chote cha masomo.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.