HALMASHAHURI YA NGORONGORO YATOA MILIONI 71 KWA VIKUNDI VYA VIJANA WANAWAKE NA WATU WENYE ULEMAVU
Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Mh.Mwl Raymond Mwangwala akabidhi mikopo ya shilingi millioni 71 kwa vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022.
Akizungumza hii leo Novemba 8,2021 katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro kwenye hafla ya utoaji wa mikopo hiyo Mh.Mwangwala amewaasa wanufaika wa mkopo huo kwenda kuitumia vizuri lengo likiwa kuwanafaisha na kuwajengea heshima katika jamii na kwenye familia,kuepusha manyanyaso mbalimbali kwa wanawake na kuleta amani ndani ya ndoa,na kuongeza kuwa wasichukue mikopo hiyo na kwenda kununulia nguo,kutoka mitoko,kuongeza mke au kuongeza mme kupitia mikopo hiyo bali wakafanye vitu vya kuwaletea maendeleo.
Kwa upande wake Afisa maendeleo ya jamii wilayani hapa Mwanamsiu Dossi akisoma taarifa fupi ya mikopo ya vikundi hivyo kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022 halmashauri imeidhinisha utoaji wa mikopo yenye jumla ya Tshs,71,000,000.00 kwa vikundi 18 vya wajasiriamali vilivyoomba mikopo kutoka mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Bi.Mwanamsiu amesema Fedha zilizokopeshwa zinatokana na mchango wa asilimia 10 ya mapato ya ndani Tshs.18,000,000.00,fedha zilizorejeshwa kutokana na mikopo ya awali Tshs.17,153,500.00 na salio la mfuko huo maalum Tshs.39,509,719.00,na kuaahidi kuendelea kutoa mikopo kwa vikundi hivyo, kulingana na fedha zitakazopatikana kutokana na makusanyo ya ndani na marejesho ya mikopo ya nyuma.
Bi,Timbiyan Kiring'oti wa kijiji cha Kirtalo kata ya Soitsambu, kutoka katika kikundi cha kunenepesha na kuuza mifugo ameishukuru halmashauri ya wilaya ya ngorongoro kwa kutoa mikopo hiyo na kuongeza kuwa fedha hiyo ya mkopo waliyoipata watakwenda kuiongeza kwenye mradi wao wa kununua na kunenepesha mifugo.
Kwa mujibu wa sheria na kanuni ya mikopo hiyo,kila kikundi kilichopata mkopo kitatakiwa kurejesha mkopo baada ya miezi mitatu tangu siku ya kupata mkopo na Marejesho ya mkopo yatafanywa kila mwezi kwa kuzingatia viwango vilivyokubaliwa kati ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa na kikundi kilichopatiwa mkopo.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.