Divisheni ya Afya Wilaya ya Ngorongoro leo tarehe 22 Februari, 2024 kimefanya kikao cha Mpango kazi na kujadili mikakati ya kutokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele, ambapo magonjwa hayo ni ugonjwa vikope (trakoma), ugonjwa wa minyoo ya tumbo na ugonjwa wa Kichocho.
Kikao kimefanyika katika Ukumbi wa Halmashauri kikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Kanali. Wilson Sakulo kisha kujadili na kuweka mikakati ya kupambana na magonjwa yasiyopewa kipaumbele katika jamii ili kuyatokomeza kabisa, kikao kimeazimia wataalamu na viongozi washirikiane kutoa elimu Kwa jamii ili kuwa na uelewa wa magongwa yasiyopewa kipaumbele na kuweza kuyakabili kwani yanaathiri maisha ya watu na kupunguza nguvu kazi katika jamii na taifa kwa ujumla.
"Kikao hiki ni muhimu sana hivyo sisi kama viongozi ni jukumu letu kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa maradhi yasiyopewa kipaumbele, pia kufahamu jinsi ya kuyadhibiti maradhi hayo kwani yanaathiri jamii yetu" amesema Kanali. Sakulo
Hata hivyo wizara ya Afya ilianzisha Idara ya uthibiti wa magongwa yasiyopewa kipaumbele januari mwaka 2009, ambapo kufikia 2015-2016 Wilaya zote nchini zilifikiwa na mpango huo na utekelezaji ukashika hatamu.
Aidha mnamo mwaka 2023 Wilaya ya Ngorongoro ilianzisha kinga tiba ya Trakoma Kwa ngazi ya Jamii ambapo kinga hiyo ilitolewa kwa awamu mbili, awamu ya Kwanza ilifanyika mwezi April na awamu ya pili mwezi Novemba 2023.
Mkuu wa Wilaya Kanal. Sakulo wakati wa hotuba yake ameendelea kubainisha kuwa,
"Tulifanikiwa kuanzisha kinga tiba Kwa ngazi ya jamii ambapo Kwa awamu ya Kwanza April tulifanikiwa kutoa kinga tiba Kwa asilimia 92 sawa na watu 209,273 huku walengwa ni 227,471 na awamu ya pili mwezi Novemba tulifanikiwa Kwa asilimia 88 sawa na watu 214,164 huku walengwa walikua ni 246,982".
Pia Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro kanali. Wilson Sakulo ameendelea kuwasihi Viongozi wa Serikali, Viongozi wa dini pamoja na Wahudumu wa afya kusimamia kwa makini suala la afya katika jamii ili kuhakikisha nguvu kazi inakuwepo wakati wa zoezi la ugawaji wa kinga tiba unaotarajiwa kuanza Februari, 2024 na awamu ya pili mwezi Octoba na Disemba, 2024.
"Ni jukumu letu sote kama Viongozi kuhakikisha afya za wananchi zinakuwa katika hali nzuri hivyo tuwaelimishe Wananchi waone umuhimu wa kushiriki katika zoezi la ugawaji kinga tiba pamoja na kutunza mazingira ili kuepusha vimelea vya maambukizi ya magonjwa mbalimbali"-Kanali. Wilson Sakulo.
Kwa upande wake Dkt. Frank Mabagala kama muelimishaji wakati wa semina fupi katika kikao hicho ameeleza sababu zinazopelekea magojwa hayo ni hali hafifu ya usafi hivyo amehimiza na kuishauri jamii kuboresha hali ya usafi kama vile kusafisha Uso kwa maji safi hususani kwa watoto ili kutokomeza trakoma, kutumia vyoo safi na bora kutokomeza homa ya minyoo ya matumbo, na kusema wataalamu wa afya wanajiandaa kutoa dawa za kichocho kuanzia tarehe 27-28 Februari, 2024 katika Shule zote za Msingi kwa Watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 14 hivyo Wananchi wanaswa kutoa ushirikiano wakati wa zoezi hilo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Dr. Revocatus Ndyekobora amebainisha Divisheni ya Afya imetenga bajeti ya kuendeshea miradi ya uthibiti wa magonjwa hayo yasiyopewa kipaumbele ili kuhakikisha huduma ya kinga tiba inawafikia walengwa kwa uhakika zaidi na kwa wakati sahihi.
Hata hivyo Viongozi wa dini nao hawakubaki nyuma katika suala hili, wamehudhuria kikao hicho na kuahidi kutoa ushirikiano katika kutoa elimu juu ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele katika nyumba zao za ibada kwa kuwahimiza waamini na waumini wao kuwa wapiganaji na kuhakikisha wanayatokomeza kabisa magonjwa hayo.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.