Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Murtallah Mbillu, ameongoza zoezi muhimu la kuogesha mifugo katika eneo la Lata Kata ya Oloipiri, linalolenga kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa ndigana baridi unaowaathiri mifugo.
Zoezi hilo limefanyika leo tarehe 14 Novemba 2024 ikiwa ni mkakati wa kuimarisha juhudi za Ufugaji ambapo Mkurugenzi ametoa msaada wa lita 12 za dawa ya kuogeshea mifugo, ambayo itawawezesha wananchi kuogesha mifugo yao bure .
Akizungumza wakati zoezi hilo, Bw. Mbillu amewasisitiza wafugaji kuogesha mifugo yao kila baada ya siku saba badala ya desturi ya kuogesha kila mwisho wa mwezi, ili kuhakikisha kinga madhubuti dhidi ya ndigana baridi.
Ameeleza kuwa afya bora ya mifugo ni muhimu kwa ustawi wa kiuchumi kwa halmashauri na wafugaji, kwani ufugaji ni nguzo kuu ya mapato ya halmashauri.
Afisa wa Kilimo, Mifugo, na Uvuvi Wilaya Bw. Chobby Chubwa, amesema katika kuhimiza wafugaji kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo, alibainisha kuwa ugonjwa wa ndigana baridi unaweza kudhibitiwa kwa njia ya kuogesha mara kwa mara.
Alieleza kuwa asilimia 70 ya magonjwa ya mifugo hutokana na kupe, hivyo kuogesha mifugo ni hatua muhimu katika kuboresha afya ya mifugo
Ndg. ambaye ni mfugaji Ramatho Saringe, kutoka kijiji cha Oloipiri, ameishukuru serikali na halmashauri kwa kuanzisha na kusimamia zoezi hilo kwani hatua hiyo itasaidia kudhibiti ugonjwa wa ndigana baridi ambao umekuwa changamoto kubwa kwa mifugo yao.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.