Ngorongoro, 19 Februari 2025 – Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Multallah Sadiki Mbillu, amewataka viongozi wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) kuondoa malalamiko ya wanufaika kuhusu malipo yao kwa kuhakikisha mfumo wa manunuzi serikalini (NeST) unatumika ipasavyo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya matumizi ya mfumo wa NeST kwa watendaji wa vijiji na CMC leo, Mbillu alisema amekuwa akipokea malalamiko ya wanufaika wa TASAF wakidai kutopata malipo yao baada ya kufanya kazi. Aidha, baadhi ya malalamiko yamedai kuwa mratibu wa TASAF anahusika na upotevu wa fedha za wanufaika, madai ambayo ameyakanusha na kusisitiza kuwa uwazi na matumizi sahihi ya mfumo wa NeST yatasaidia kuondoa changamoto hizo.
Kwa upande wake, Mratibu wa TASAF Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Thomas Nade, alieleza kuwa wanufaika wa ajira za muda chini ya miradi ya TASAF watafanya kazi kwa mikono kwa muda wa masaa manne kwa siku kumi ndani ya mwezi na kulipwa kiasi cha Tsh 30,000, ambapo kila siku watapata Tsh 3,000. Aliwataka watendaji wa vijiji kufanya kazi kwa kujitolea ili kusaidia kaya maskini badala ya kutanguliza maslahi binafsi.
Kuhusu utekelezaji wa miradi ya TASAF kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Bw. Nade alisema wilaya ya Ngorongoro imepokea Tsh 904,743,147.5 ambazo zinatumika kutekeleza miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa nyumba ya mwalimu katika Shule ya Msingi Wasso, malambo, bweni katika Shule ya Sekondari Digodigo, jengo la OPD katika Zahanati ya Soitsambu, pamoja na nyumba za madaktari katika vijiji vya Ormanie na Tinaga.
Mafunzo hayo yamepokelewa vyema na washiriki, ambapo Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Loswash, Bw. Ally Mrisho, alisema mafunzo ya NeST yatasaidia kuhakikisha wanufaika wa TASAF wanapata malipo yao kwa wakati. Bi. Likya Peter, Msimamizi Msaidizi wa Miradi ya TASAF katika kijiji cha Ololosokwan, aliishukuru serikali kwa mfumo huo mpya, akisema utapunguza muda wa kutafuta nukuu za bei za bidhaa kutokana na changamoto za kijiografia za vijiji vyao.
Mafunzo haya yanatarajiwa kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya TASAF, kuhakikisha kuwa wanufaika wanapata haki zao bila changamoto.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.