Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Kanali Wilson Sakulo amefanya ziara ya kutembelea Wananchi wa kata ya Sale na Engarasero leo tarehe 25 Septemba, 2024 kwa lengo la kufanya kampeni ya kuhamasisha kushiriki katika zoezi la kujiandikisha katika daftari la mpiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa litakalofanyika kwa muda wa siku kumi.
Katika ziara hiyo Wananchi wa kata hizo wamehaswa kuhamasishana wenyewe juu ya umuhimu wa kujiandikisha na kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwani ni haki ya kikatiba ya kila mtanzania mwenye vigezo na kushiri katika masuala ya uchaguzi kwani inawapa fursa ya kumchagua kiongozi wanayemuhitaji kwa manufaa yao.
"Nina imani na uhakika siku ya kujiandikisha ya tarehe 11 hadi 20 Oktoba mwaka huu, mtajitokeza kwa wingi kujiandikisha na kutekeleza haki yenu ya msingi kwani kila mmoja wetu hapa ni mzalendo na ninatoa rai kila mmoja amuhamasishe mwenzie kujitokeza kujiandikisha" amesema Mhe. Kanali Sakulo.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ameongeza kwa kusema kuwa kila mwananchi lazima ajiandikishe kwenye kitongoji au kijiji ambacho ndio makazi yake.
"Kila mmoja atajiandikishia mahali anapotokea au kuishi na ndio sehemu hiyohiyo atakapokwenda kumchagua kiongozi anayemtaka kama umejiandikishia Engarasero au umejiandikishia Sale basi ndio hapo hapo utakapo pigia kura yako hili nalo nimeona niliweke sawa ili kuondoa mkanganyiko".
Pia, wakati wa mkutano Wananchi wametakiwa kushiriki pia katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika rasmi tarehe 27 Novemba 2024 nchi nzima.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.