Mkuu wa polisi Wilaya ya Ngorongoro Leah Ncheyeki ametoa wito wa kuwataka Wananchi kuwa mstari wa mbele kupinga masuala yanayopelekea ukatili kila mmoja kusimama kwenye nafasi yake ili kuliondoa suala hili kwenye jamii, amesema hayo wakati kikao cha kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kilichofanyika leo tarehe 10 Desemba, 2024 katika ukumbi wa mkutano wa Halmashauri.
Wadau waliohudhuria kikao hicho ni wamiliki wa nyumba za kulala wageni, maafisa wasafirishaji (bodaboda) na wamiliki wa baa, huku wakitakiwa wao pamoja na wananchi wengine kuungana kwa pamoja kulivaa jukumu la kupinga ukatili wa kijinsia kwenye jamii.
0
Aidha, OCD Leah amesema kuwa suala ukatili wa kijinsia sio kwa watoto na wanawake pekee bali hata wanaume hukutwa na janga hili ni vyema sasa jamii ikaanza kuchukua hatua.
"Chukua hatua ukatili wa kijinsia hauvumiliki hata kidogo, hivyo sisi tuwe sehemu ya kuwalinda watoto, tulibebe hili kama jukumu letu. Ibada njema huanzia nyumbani hivyo tusimame kwenye nafasi zetu kupinga ukatili wa kijinsia" ameongeza OCD Leah Ncheyeki.
Sambamba na hilo, Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya Bw. Bennezeth Bwikizo ametumia fursa hiyo kutoa elimu kupinga ukatili kwa wadau na nini cha kufanya waonapo viashiria vya matendo ya ukatili kwenye jamii, amesema inatakiwa ifike mahali Ngorongoro iwe sehemu salama ya kuishi pasipo kuwepo na kesi za ukatili wa aina yoyote.
"Niwaombe wadau wote tushirikiane, ikiwa utaona tukio au tendo lolote linaloashiria ukatili toa taarifa kwenye mamlaka husika ili lifanyiwe kazi mapema na haraka ili kuilinda jamii kwa kufanya hivyo utakua umekataa ukatili kwa nafasi yako na mwisho tutakua na jamii salama".Amesema Bw. Bennezeth.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.