NGORONGORO:.
16.02.2022
Baraza la Madiwani halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro limepitisha Mpango wa Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka ujao wa fedha 2022/2023, kwenye mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani ulliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro, mheshimiwa Marekani Bayo, amethibitisha baraza hilo kupitisha Mpango wa bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka ujao wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 33.4,kwa kuwataka watalamu, kuboresha vyanzo vya mapato vilivyopo na kuimarisha mkakati wa ukusanyaji mapato huku wakiendelea kubuni vyanzo endelevu vya mapato vitakavyowezesha utekelezaji wa bajeti iliyopitishwa kiuhalisia.
"Ninawapongeza watalamu wa ngazi zote, ofisi ya mkuu wa wilaya ya Ngoromgoro, waheshimiwa madiwani na wadau wote wa maendeleo kwa ushirikiano wao unaowewezesha kusukuma gurudumu la maendeleo la halmashauri yetu, licha ya changamoto nyingi lakini bado utekelezaji wa malengo ya halmashauri unafanyika kwa kasi" amesema Mheshimiwa Mwenyekiti huyo.
Aidha Mwenyekiti huyo, ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuendlea kuleta fedha za kutekeleza miradi mikubwa katika halmashauri hiyo, ikiwemo miradi ya maji, barabara, umeme, elimu na afya, miradi ambayo kupitia mapato ya halmashauri peke yake isingeweza kutekelezeka
Awali akiwasilisha Rasimu ya Mpango wa Bajeti ya Mapato na Matumizi ya kwa mwaka ujao wa fedha 2022/2023 mbele ya wajumbe wa Baraza la Waheshimiwa Madiwani, Afisa Mipango halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro , Bi Emmy Hongoli amesema kuwa, halmashauri inategemea kukusanya na kutumia jumla ya shilingi bilioni 33.4 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato.
Afisa Mipango huyo ameainisha mchanganuo wa bajeti hiyo ya bilioni 33.4 itahusisha mapato ya ndani kiasi cha shilingi bilioni 2.3 Ruzuku ya mishahara (PE) shilingi bilioni 13.5 Ruzuku ya matumizi mengine (OC) shilingi milioni 700 huku Ruzuku ya Miradi ya Maendeleo ikiwa ni shilingi bilioni 16.8
Hata hivyo Afisa Mipango huyo, amesema kuwa mpango huo wa bajeti umeandaliwa kwa mujibu wa kifungu Na. 11 cha sheria ya Sheria ya Bajeti Na. 21 ya mwaka 2015 pamoja na Kanuni zake, maelekezo na mwongozo wa kitaifa maandalizi ya Bajeti, unaoelekeza kupokea mapendekezo na vipaumbele kisekta kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata, Idara na Vitengo vya halmashauri.
Ameongeza kuwa, halmashauri imefanya Mpango wa Bajeti hiyo, kwa kuzingatia ukomo wa bajeti na kwa mujibu wa Sheria na Maelekezo na Mwongozo wa kitaifa lakini pia imezingatia Mpango shirikishi wa Jamii, Mpango mkakati wa halmashauri wa mwaka 2021/2022 mpaka 2025/2026 na vipaumbele vya halmashauri kisekta kwa kuzingatia maeneo
Aidha Afisa Mipango Ana ameendelea kufafanua kuwa, katika mpango huo wa Bajeti umejikita pia katika kutekeleza shughuli zinazolenga kutekeleza Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania ( MKUKUTA III), inayosisitizwa na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, Mpango wa Taifa wa Miaka mitano , Malengo ya maendeleo endelevu, (SDG's) ya 2030 pamoja na kuzingatia 'Tanzania Development Vission 2025'.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.