Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. kanali Wilson Sakulo ameshiriki na kuongoza kikao cha tathmini ya utelezaji wa shuguli za lishe kwa kipindi cha miezi mitatua kuanzia mwezi Aprili hadi Juni 2024 leo tarehe 31 Julai, 2024 katika ukumbi mdogo wa Halmashauri.
Hali ya lishe kwa Watoto imeendelea kuimarika kutokana na kuongezeka kwa asilimia za hali nzuri ya lishe kuendelea kupanda ukilinganisha na vipindi vilivyopita.
Afisa lishe Bi. Angela Mbaga wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha mwezi Aprili mpaka Juni 2024, amesema jumla ya Watoto 35,503 walifanyiwa tathmini ya hali ya lishe huku idadi ya Watoto 33,004 sawa na asilimia 92.96 walikutwa na hali nzuri ya lishe na asilimia 6.79 sawa na watoto 2, 410 walikutwa na hali ya hafifu ya lishe.
Bi.Angela Mbaga ameendelea kueleza kwa kipindi chote cha miezi mitatu walifanya maadhimisho ya siku ya afya na lishe katika kata nane (8) ikiwemo Oloipiri, Endulen, Samunge, Kirangi, Orgosorock, Olorien, Enguserosambu na Maalon, maadhimisho hayo yalihusisha utoaji wa huduma za kliniki ya mkoba, upimaji wa hali ya lishe kwa watu wazima na kutoa ushauri na nasaha kuhusu lishe bora.
Sanjari na hilo jumla ya akina mama 5, 940 walipatiwa elimu ya lishe ya makundi ya chakula, uandaaji wa mlo kamili na chakula cha nyongeza kwa watoto.
Pia utoaji wa vidonge vya madini chuma kwa akina mama wajawazito vilitolewa ili kuendelea kuboresha hali ya afya timamu kwa wajawazito.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Wilaya Mhe. Kanali Wilson Sakulo ametoa rai kwa Watendaji wa kata kuendelea kusimamia vyema shughuli za lishe katika kata zao ili kuhakikisha Wilaya inaendelea kuwa na watoto wenye hali nzuri ya lishe.
"Licha yakuwa tuna viashiria vizuri vya hali ya lishe, sitapenda kuona watu wanalipana posho halafu hakuna kinachofanyika hivyo Watendaji kasimamiaeni vizuri shughuli za utekelezaji wa masuala ya lishe kwenye kata zenu" amesema Mhe. Kanali Sakulo
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya amewahimiza Watendaji kuwa na ushirikiano wenye tija na vikundi vya wanawake wajane vilivyopo katika kata zao ili kujenga jamii yenye upendo.
Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Ngorongoro kupitia wataalamu na uwezeshaji kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji ilifanya zoezi la utoaji wa matone ya vitamin A na dawa za minyoo katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya na kliniki za mkoba ambapo jumla ya watoto 51,115 kati ya 54,898 walifikiwa.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.