SENSA YA WATU NA MAKAZI 2022
Tanzania itafanya Sensa ya watu na makazi 23 Agosti mwaka 2022 siku iliyotangazwa na Mh. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. Kabla ya zoezi la kuhesabu watu wote watakaolala ndani ya mipaka ya nchi usiku wa kuamkia siku ya Sensa, shughuli mbalimbali za maandalizi hufanyika ambazo hujumuisha utoaji Elimu kwa lengo la kuelimisha umma juu ya umuhimu wa Sensa ili kuhakikisha kila mmoja anatambua umuhimu wa kuhesabiwa na kuhamasika kuhakikisha kwamba anahesabiwa na anahesabiwa mara moja tu.
Elimu hii inajumuisha mada mbalimbali zikiwemo; Sensa ni nini, Nani anapaswa kuhesabiwa, ni taarifa gani zitakusanywa wakati wa Sensa na umuhimu wa kuweka kumbukumbuku za watu wote waliolala katika kaya usiku wa kuamkia siku ya Sensa. Mambo muhimu unayopaswa kuyafahamu kuhusu Sensa ya Watu na Makazi ni yafuatayo:
Sensa ya watu na makazi ni moja ya zoezi linalokusanya taarifa za kila mtu aliyelala ndani ya mipaka ya nchi usiku wa kuamkia siku ya Sensa. Sensa ya Mwaka 2022 kama zilivyo Sensa zilizopita,itahusisha Makarani wa Sensa ambao watatembelea kaya zote nchini na kufanya Mahojiano ya ana kwa ana baina ya Karani wa Sensa na Mkuu wa kaya. Ikiwa Mkuu wa kaya hatakuwepo, karani wa Sensa atafanya Mahojiano na mtu mzima yeyote katika kaya ambae ana taarifa za kutosha kuhusu kaya na wanakaya wenzake waliolala katika kaya husika usiku wa kuamkia siku ya Sensa.
Lengo la Sensa ya watu na makazi ni kupata taarifa sahihi za Kidemografia, Kijamii, Kiuchumi na hali mazingira kwa lengo la kupata takwimu sahihi zitakazoiwezesha serikali na wadau wengine kupanga kwa usahihi mipango ya maendeleo ya watu wake katika sekta mbalimbali za Elimu, Afya, hali ya Ajira ,miundombinu kama barabara, Nishati na maji safi. Kwa msingi huo, Sensa ni zoezi muhimu ambalo kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kushiriki na kutimiza wajibu wake ili kuhakikisha inakuwa ya mafanikio makubwa. Hii itasaidia serikali kutimiza wajibu wake kwa wananchi kulingana na idadi ya watu ya eneo husika ikiwa kama msingi mkubwa wa ugawaji ya keki ya Taifa kwa kila eneo la utawala hapa nchini.
Sensa yam waka 2022 kama zilivyo Sensa zilizopita, itafanyika nchi nzima na itahusisha watu wote watakaolala ndani ya mipalaka ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. Hii inamaanisha kuwa, watu wote watakaolala katika kaya binafsi usiku wa kuamkia siku ya Sensa pamoja na watu wote watakaokuwa katika kaya za jumuiya kama vile hotelini , nyumba za kulala wageni, hospitalini, magereza, mabweni ya wanafuni, kambi za jeshi, vituo vya kuleelea watu wenye mahitaji maalum kama yatima, wazee, kambi za wavivu, watu wasio na makazi maalum,na vituo vya usafiri wa umma (kama vituo vya mabasi, garimoshi, viwanja vya ndege na bandari) watahesabiwa kwa kutumia utaratibu maalum utakaondaliwa na kamati ya Sensa katika ngazi ya mtaa, kitongoji na shehia.
Unachotakiwa kufanya ni kumpa ushirikiano wa kutosha karani wa Sensa atakapokutembelea katika kaya kwa kujibu maswali yote atakayouliza kwa usahihi. Aidha,ukiulizwa swali na hujalielewa au hujasikia vizuri,unayo haki ya kumwomba karani arudie kuuliza au kutoa ufafanuzi ili uweze kutoa jibu sahihi kulingana na swali lililoulizwa. Ni muhimu kwa Mkuu wa kaya kuhakikisha anachukua taarifa muhimu (kama umri, elimu, jinsi, hali ya ndoa, umiliki wa vitambulisho wa Taifa, shughuli za kiuchumi) za watu wote waliolala katika kaya yake usiku wa kuamkia siku ya Sensa ili aweze kukumbuka wakati karani atakapokutembelea katika kaya.
Siku ya Sensa, Karani wa Sensa akiongozana na Mwenyekiti au kiongozi wa Serikali ya Mtaa au Kitongoji/Shehia atafika katika kaya akiwa na kitambulisho cha Karani wa Sensa na Dododso la Sensa lililowekwa katika kifaa cha kielektroniki kiitwacho kishikwambi (Tablet) na kuuliza maswali ambayo yatajibiwa na Mkuu wa kaya. Ikiwa mkuu wa kaya hayupo, mtu mwingine yeyote mzima katika kaya ambaye ana taarifa za kutosha kuhusiana na kaya na watu wote waliolala ndani ya kaya husika usiku wa kuamkia siku ya Sensa anaweza kujibu maswali ya Sensa kwa niaba yake.
Taaridfa zitakazokusanywa zitahusu:
Ndio, kama ambavyo hufanyika katika Sensa na tafiti nyingine za kitakwimu, kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu sura 351, taarifa utakazotoa kwa karani wa Sensa zitakuwa SIRI na zitatumika kwa madhumuni ya kitakwimu pekee. Kwa mujibu wa sheria hii, kila karani wa Sensa atasaini kiapo cha kutunza siri za taarifa zote atakazokusanya na chini ya kiapo hicho hatakiwi kutoa taarifa alizotumwa kukusanya kwa mtu yeyote Zaidi ya kuziwasilisha kama zilivyo katika Ofisi ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar. Karani yeyote akithibitika kwenda kinyume na kiapo cha kutunza siri, atashitakiwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria hii.
Karani wa Sensa atafika katika kaya akiwa na kitambulisho na sare maalum inayomtambulisha. Pia ataongozana na Mwenyekiti au kiongozi wa serikali ya Mtaa/kitongoji/shehia.
Ndio, kujibu maswali ya Sensa ni matakwa ya Kisheria kwa mujibu wa sharia ya Takwimu sura namba 351.
Kumbuka: Ushirikiano wako wa karani wa Sensa na Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa kutoa taarifa sahihi ndio utakaorahisisha na kufanikisha Sensa ambapo matokeo yake yatachochea kasi ya maendeleo ya watu na makazi yao katika maeneo yote ya utawala nchini.
Hapana, UVIKO-19 siyo kikwazo kwa yeyote kushiriki kwa nafasi yake katika Sensa ya mwaka 2022 kwani kulingana na maendeleo ya ugonjwa huu, makarani na watendaji wote katika Sensa hii watazingatia tahadhari zote zinazoelekezwa na Wataalamu wa Afya ili kutokuwaambukiza wananchi au wao kuambukizwa na wananchi wakati wa zoezi la Sensa.
Shiriki kikamilifu sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa maendeleo endelevu ya Tanzania
SENSA KWA MAENDELEO,
JIANDAE KUHESABIWA
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.