Ngorongoro ,Arusha
02 Dec 2018
Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imefanya zoezi la kufanya ufuatiliaji wa marejesho ya mikopo iliyotolewa kwa vikundi vya ujasiriamali vya vijana na wanawake Tarafa ya Ngorongoro. Kata zilizotembelewa ni Olbalbal, Ngoile, Kakesiyo, Alaitole, Endulen, Oloirobi, na Nainokanoka.
Akizungumza na Kaimu Afisa Habari Gabriel Mpeho, Afisa Maendeleo ya Jamii (W) Bi. Teresia A Irafay, amewashukuru wadau hasa Waheshimiwa Madiwani na wenyeviti wa vijiji pamoja na Maafisa Watendaji wa kata na vijiji katika kutoa ushirikiano wa karibu kwenye uhimizaji wa marejesho. Katika shughuli hiyo, Bi Teresia aliambatana na Afisa Urithi Mambo Kale, Bi. Lightness Kyambile ambae pia ni Mratibu wa Mradi wa Geopark – Mradi unaolenga kuwezesha wanavikundi wanaojishughulisha na masuala ya utalii wa asili kwenye vivutio vinavyoratibiwa na Ngorongoro Lengai UNESCO Global Geopark.
Hali ya marejesho kwa mujibu wa Afisa Maendeleo ya Jamii (W), unaridhisha. Jitihada za makusudi zinaendelea kufanyika ili marejesho hayo yafanyiike kwa kiwango cha juu zaidi ili vikundi vingine viweze kupata fursa za kukopeshwa.
Aidha Bi Teresia anatoa rai kwaWaheshimiwa Madiwani, wajumbe wa serikali za vijiji na Maafisa watendaji wote kuendelea kutoa ushirikiano katika kuratibu shughuli za vikundi pamoja na uratibu kwenye urejeshwaji. Idara inaendelea kuboresha mifumo ya urejeshwaji na utoaji wa mikopo.
Pamoja na hayo, amekumbusha wadhamini wa vikundi kuwa makini kwani wao ndio watawajibika kisheria endapo vikundi vikikiuka mkataba kwa kuchelewesha marejesho. Hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao kwa niaba ya wanavikundi ikiwa ni pamoja na kuwapeleka mahakamani.
Afisa Maendeleo pia amewapongeza na kuwashukuru wataalamu wote wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha, Mkurugenzi Mtendaji (W) ya Ngorongoro, Bw. Raphael Siumbu na Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango pamoja , Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Baraza la Wafugaji kwa kuona umuhimu wa kuwezesha vikundi vya ujasiriamali na hatimaye Mkoa wa Arusha kwa ujumla umeshika nafasi ya kwanza kati ya Mikoa 25 ya Tanzania Bara katika kuwezesha vikundi vya ujasiriamali kupitia 10% ya Mapato yake ya ndani na vyanzo vingine kutoka kwa wadau wa maendeleo.
Amewashukuru Maafisa Maendeleo ya Jamii wote pamoja na watenadaji wa kata na vijiji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na waliopo Baraza la Wafugaji kwa kazi nzuri wanayofanya vijijini na kuendelea kuwatia moyo katika kuhudumia wananchi na kuwa wabunifu zaidi katika kutekeleza majukumu yao.
Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro
Afisa Maendeleo ya Jamii (W)Ngorongoro Bi.Teresia A.Irafay na Afisa Mambo Kale wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bi Lightness Kyambile wakiwa katika Picha ya Pamoja na wajumbe wa serikali ya kiijiji cha Ngoile baada ya Majadiliano ya kina kuhusu maendeleo ya vikundi na urejeshwaji wa mikopo
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.