Wananchi wa Wasso na Loliondo Wilaya ya Ngorongoro wametakiwa kulinda afya kwa kufuata na kuzingatia kanuni bora za lishe kupitia vyakula wanavyokula ili kuepukana na changamoto za magonjwa pamoja na udumavu katika jamii.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtandaji Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro Bw. Bennezeth Bwikwizo wakati wa akifungua mkutano wa Maadhimisho ya siku ya Lishe kitaifa ambapo kiwilaya yamefanyika leo tarehe 30 Oktoba, 2024 katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Hata hivyo, Bw. Bennezeth Bwikwizo amewaasa Wananchi waliohudhuria katika maadhisho hayo waende wakawe mabalozi wazuri kwenye jamii kwa kuhimizana wao wenyewe kuzingatia ulaji bora wenye kuzingatia vyakula vyenye virutubisho ili kutengeneza jamii yenye kizazi makini na chenye afya njema.
"Ili tuwe na kizazi chenye afya bora lazima tuboreshe ulaji wetu, ndio maana Rais wetu kwa kulitambua hilo ameweka nguvu kubwa sana kwenye eneo la lishe. Hivyo lazima tuondoe udumavu wa akili na mwili kwetu sisi wenyewe na vizazi vyetu kwa kuzingatia lishe inayofaa ndio maana nawaambieni kaweni mabalozi wazuri kwenye jamii yetu, niwahakikishie vita hii tutaishinda"
Pia, Afisa Lishe Wilaya ya Ngorongoro Bi. Angela Mbaga ametumia fursa hiyo kama njia ya kutoa elimu juu ya lishe bora kwa kufundisha namna bora ya kuandaa unga wa lishe wenye virutubisho vyote muhimu katika afya ya ukuaji wa mtoto ambavyo utaweza kusaidia kuimarisha utimamu wa akili na mwili wa mtoto.
Aidha, elimu ya afya na akinamama wajawazito imetolewa ambapo wametakiwa kuzingatia matumizi ya dawa za madini chuma ili kuboresha utimamu wa mwili wa mama, pia wametakiwa kuwa wanahudhuria vituo vya afya kipindi chote cha ujauzito na kufika hospitali au kituo chochote cha Afya wakati wa kujifungua na kuachana na tabia ya kujifungulia nyumbani.
Sanjari na hayo, elimu ya uanzishaji wa bustani za mbogamboga imetolewa na kuwahamasisha Wananchi kuwa ni muhimu kila mwananchi akaanzisha bustani ndogo ya mboga katika eneo lake kama njia ya kupata virutubisho kamili kutoka kwenye mboga hizo na kuepuka matumizi ya mboga zenye matumizi makubwa ya dawa zenye kemikali, ambapo elimu ya kutumia eneo dogo kulima mbogamboga kwenye eneo dogo kwa kutumia mbinu za kisasa.
Elimu hiyo imetolewa na Bw. Tonny Alfred Mwakifwamba Afisa umwagialiaji Wilaya kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji. Maadhimisho hayo yalikua na kauli mbiu inayosema "Mchongo ni Afya yako, Zingatia Unachokula".
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.