Chanzo na Elinipa Lupembe-OFISI YA MKUU WA MKOA ARUSHA.
Wanafunzi 5,298 Mkoa wa Arusha, wameanza kufanya Mtihani wa kuhitimu kidato cha sita leo Mei 06, 2024 nchini, kwa mujibu wa ratiba ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
Akizungumza na mwandishi wetu, Afisa Elimu Mkoa wa Arusha, Mwl. Abel Mtupwa amesema kuwa, idadi hiyo ya Wanafunzi, inajumuisha Watahiniwa wa Shule, Watahiniwa wa kujitegemea pamoja na Watahainiwa wa Ualimu ngazi ya Cheti na Stashahada.
Amefafafanua kuwa kati ya Watahiniwa 5,298, Watahiniwa 4,286 ni wa shule 'School candidates', Watahiniwa 450 ni wa kujitegemea 'Private Candidates' na Watahiniwa 562 ni wa Ualimu.
Mwl. Mtupwa amebainisha kuwa, Watahiniwa wote watafanya mitihani yao, kwenye vituo rasmi 62 na vituo teule ni 23, huku kukiwa na jumla ya Wasimamizi Wakuu 61 na Wasimamizi wa Mikondo 135.
"Maandalizi yamekamilika kwenye vituo vya kufanyia mitihani, vifaa vyote vya muhimu vimepokelewa kwa utoshelevu wake kutoka Baraza la Mitihani la Tanzania na tayari Semina elekezi kwa ajili ya kufanikisha kazi hii ya kitaifa zimefanyika kwa ufasaha kwa Wasimamizi wote" Amesema Mwl. Mtupwa
Hata hivyo amewataka Wasimamizi wote wa mitihani, kufanya kazi hiyo kwa uadilifu kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za mitihani ya Taifa, sambamba na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuathiri uendeshaji wa mitihani uliopangwa na Serikali, kwa kuwa tayari wanafunzi wameshaandaliwa vyema na walimu wao kwa shule zote.
Aidha, mitihani hiyo imeanza leo Mei, 6 na inatarajiwa kumalizika Siku ya Ijumaa ya tarehe 24 Mei 2024.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.