Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro chini ya Bw. Nassoro Shemzigwa, imeendelea kusisamamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita inayoongonzwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha Mhe. Loy Ole Sabaya leo tarehe 4 machi, 2024 ameiongoza Kamati ya Siasa ya Mkoa kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa Wilayani Ngorongoro, na kutoa pongezi kwa miradi inayoridhisha katika utekelzaji ikiwemo Shule ya Sekondari Masusu ambayo imekamilika kisha kutoa maagizo ya ukamilishwaji kwa miradi yote ili kuhakikisha utendaji kazi unaenda vizuri na miradi inakamilika kwa wakati.
Shule ya Masusu imegharimu kiasi cha shilingi milion 584.2, Shule hiyo ina madarasa 8, Ofisi 2, jengo la utawala, maabara ya Kemia, fizikia, baiolojia, jengo moja la maktaba na jengo la TEHAMA
Aidha Mwenyekiti ametoa pongezi kwa Wananchi wa Kata ya Pinyinyi na Uongozi wa Halmashauri kwa juhudi walizozifanya kuhakikisha Shule ya Sekondari Masusu inakamilika.
"Nitoe pongezi kwa umoja wenu na juhudi mlizozifanya mpaka kuhakikisha ujenzi wa Shule hii unakamilika hongereni sana, pia hakikisheni watoto wanaenda shule mpaka wamalize masomo yao ili baadaye wawasaidie." amesema Ole Sabaya.
Hata hivyo amemtaka Meneja wa mamlaka ya maji Vijijini (RUWASA) Mhandisi Gerald Patrick Andrew kuhakikisha anatimiza ahadi yake ya kufikisha huduma ya maji siku ya Ijumaa ya tarehe 8 machi, 2024.
Agizo hilo limekuja baada ya Meneja wa RUWASA kusema mpaka kufikia ijumaa huduma ya maji itakua inapatikana shuleni hapo wakati akijibu hoja ya mwanakijiji wa Masusu inayodai kuwa huduma ya maji Shuleni hapo ni changamoto.
Kamati ya Siasa imetembelea miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa Katika Kata ya Maaloni ikiwemo barabara ya Kipambi yenye urefu wa kilomita 14.6 iliyogharimu kiasi cha shilingi bilion 3.1 za kitanzania, ujenzi wa madarasa mawili Shule ya Msingi Kipambi kisha barabara ya Ormanie hadi Olala yenye urefu wa kilomita 9.33 inayojengwa kwa hisani ya benki ya maendeleo ya Ujerumani (KFW) Kata ya Arash.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.