Kikao cha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe ngazi ya Halmashauri kimefanyika leo tarehe 25 Julai, 2025, kwa lengo la kujadili taarifa za shughuli za lishe zilizotekelezwa katika robo ya nne, kuanzia mwezi Aprili hadi Juni 2025. Lengo kuu la kikao hiki ni kutathmini hali ya lishe ndani ya Wilaya ya Ngorongoro na kubaini mwelekeo wa utekelezaji wa afua za lishe.
Katika kikao hicho, taarifa iliyowasilishwa ilionyesha kuwa jumla ya watoto 64,084 wenye umri chini ya miaka mitano walipimwa uzito na hali ya lishe katika kliniki za mama na mtoto. Pia, maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe yamefanyika hadi kufikia ngazi ya vijiji. Aidha, jumla ya wanawake wajawazito 15,758 walipatiwa vidonge vya madini chuma.
Afisa Lishe wa Wilaya, Bi. Angela Mmbaga, akiwasilisha taarifa hiyo kwa wajumbe wa kikao, alisema kuwa ukaguzi wa vyakula na upimaji wa afya katika migahawa na hoteli umefanyika, sambamba na ukaguzi wa mifugo na utoaji wa elimu ya kilimo kwa vikundi mbalimbali vya jamii.
Kuhusu hali ya lishe kwa watoto chini ya miaka mitano, Bi. Angela alieleza kuwa jumla ya watoto 24,001 wa jinsia ya kiume walikutwa na hali nzuri ya lishe, huku watoto 25,823 wa jinsia ya kike wakionyesha hali hiyo hiyo. Hii inafanya jumla ya watoto waliokuwa na hali nzuri ya lishe kuwa 49,824, sawa na asilimia 95.5 ya walipopimwa.
Maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe ya Vijiji yalifanyika katika kata nane (8) kati ya saba (7) zilizopangwa awali, ambazo ni: Enguserosambu, Orgosorok, Maalon, Ngoile, Ngorongoro, Samunge, Kirangi na Olorien/Magaidiru. Kikao hicho kimeongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri, Bw. Bennezeth Bwikizo, katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.