Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya lami ya Mto wa Mbu–Engaruka–Ngaresero, yenye urefu wa kilomita 74, itakayounganisha wilaya za Monduli na Ngorongoro. Mradi huu unalenga kukuza shughuli za kiuchumi na kijamii, hususan sekta za utalii na uwekezaji mkoani Arusha.
Akizungumza wakati akihitimisha ziara yake wilayani Monduli Septemba 10, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA Amos Gabriel Makalla amesema usanifu wa barabara hiyo umekamilika na hatua za kumpata mkandarasi zimeanza. Amesema ujenzi huo utarahisisha uwekezaji kwenye kiwanda cha magadi soda cha Engaruka na kuimarisha utalii kupitia vivutio kama Ziwa Natroni.
Makalla alibainisha kuwa barabara hiyo itajengwa kwa vipande vitatu: kilomita 23 za Mto wa Mbu–Selela, kilomita 27 za Selela–Engaruka na kilomita 24 za Engaruka–Ngaresero. Amewataka viongozi wa wilaya hizo kusimamia kikamilifu mradi huo pamoja na miradi mingine ili ikamilike kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.
Mbali na barabara, Makalla alieleza kuwa Rais Samia pia ametenga shilingi bilioni 17 kwa ajili ya mradi wa umwagiliaji wilayani Monduli, unaotarajiwa kunufaisha vijiji zaidi ya 11. Amesema mkandarasi wa mradi huo tayari amepatikana na utekelezaji utaanza muda mfupi ujao.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.