Katibu Tawala Wilaya ya Ngorongoro amefungua na kuongoza kikao cha tathmini ya utekelezaji wa afua za lishe Wilaya, kilichofanyika leo tarehe 27 Juni, 2024 katika ukumbi wa Halmashauri ambapo kikao hicho kimehudhuriwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo Watendaji wa Kata, Wataalamu kutoka Halmashauri, maafisa lishe, pamoja na kamati ya usalama ya Wilaya.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya tathmini ya lishe Afisa Lishe Wilaya Bi. Anjela Mbaga ameeleza kuwa watoto 32, 153 walifanyiwa tathmini ya lishe kwa kupimwa uwiano wa uzito na urefu kwa umri kupitia vituo vya kutolea huduma ya afya, Watoto 29, 334 sawa na asilimia 91.23 walikua na hali nzuri ya lishe. watoto 2, 734 sawa na asilimia 8.5 waligundulika kuwa na hali hafifu, watoto 85 sawa na asilimia 0.26 waligundulika walikua na hali mbaya ya lishe.
"watoto hao walipewa chakula dawa, na walezi walifundishwa aina gani ya chakula wanatakiwa kuwaandalia watoto hao ili waweze kurejea katika hali ya kawaida" amesema
Bi. Anjela wakati akitoa maelezo kuhusu hatua zilizochukuliwa na Wataalamu wa lishe ili kurejesha hali nzuri ya lishe kwa Watoto waliogundulika kuwa na hali hafifu na wale wenye hali mbaya ya lishe.
Hata hivyo, aliendelea kueleza kuwa kwa kipindi cha januari hadi machi utoaji wa vidonge vya madini chuma uliendelea kutolewa huku jumla ya akinamama 10, 453 kati 10, 462 sawa na asilimia 99.9 walipatiwa vidonge vya madini chuma katika kliniki za mama na mtoto.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya Ndg. Hamza H. Hamza amekipongeza kitengo cha lishe kwa utekelezaji mzuri wa kutoa huduma ya lishe bora kwa Watoto na akina mama wajawazito, pia amempongeza Mkurugenzi Mtendaji kwa kuwawezesha Maafisa Lishe kutekeleza majukumu yao kikamilifu wakati wote wa utekelezaji wa zoezi la utoaji huduma ya lishe kwa maeneo yote wilayani Ngorongoro.
Aidha, Katibu Tawala amesema katika kuboresha hali ya lishe wilayani amewataka Maafisa Elimu, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Kilimo na Watendaji wa Kata kuhamasisha ulimaji wa bustani za mbogamboga kwenye maeneo yao ili kuendeleza na kuboresha hali ya afya timamu kwa watoto.
"Tuendelee kufanya kazi na tuendelee kuhamasisha, suala la lishe sio suala la lelemama hakuna namna ambayo tunaweza kuikwepa lishe kama tunataka kuwa na kizazi kinachokua kwa uelewa mkubwa" amesema Ndg. Hamza
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.