Mnamo tarehe 16-12-2017 kamati ya Michezo Wilaya iliandaa mashindano ya loliondo - serengeti half marathon. Lengo la mashindano haya lilikuwa kusherehekea miaka 56 ya uhuru wa Tanzania bara, kuimarisha afya, kuinua ari ya michezo Ngorongoro, kuibua vipaji mbalimbali pamoja na kuhamasisha wananchi kuhifadhi mazingira na kulinda maliasili zilizopo kwa lengo la kuendeleza utalii Ngorongoro ili tuweze kunufaika kama wilaya pia kama Taifa. Mashindano haya yaliongozwa na kauli mbiu isemayo tushiriki kulinda na kuhifadhi maliasili kwa pamoja ili kukuza utalii kwa maendeleo yetu. Mashindano haya yalihusisha michezo mbalimbali ikiwemo riadha na mpira wa miguu. Kwa upande wa riadha wananchi walikimbia mbio za kilometa 21 kwa wanaume , kilometa 10 kwa wanawake na kilometa 2.5 kwa watoto.
Mgeni rasmi katika mashindano haya alikuwa Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro ndugu Rashid M. Taka. Mgeni rasmi aliambatana na kamati ya ulinzi na usalama na viongozi wengine akiwemo Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Ngorongoro ndugu Raphael J. Siumbu , wakuu wa idara, watumishi wengine wa halmashauri, taasisi za umma na binafsi. Mashindano haya pia yalihudhuriwa na mwenyekiti wa CCM Wilaya.
Uzinduzi wa mbio hizo ulianza mapema asubuhi kwa mbio za viongozi ambapo mheshimiwa Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi mtendaji wa halmshauri ya wilaya ngorongoro waliongoza mbio hizo. Baada ya hapo mashindano yalianza rasmi ambapo mbio za kilometa 21 wanaume walikimbia Kuanzia shule ya msingi wasso kupitia barabara ya sakala hadi loliondo NMB junction na kurudi shule ya msingi wasso kupitia barabara kuu. Wanawake kwa mbio za kilometa 10 walikimbia kuanzia shule ya msingi wasso hadi shule ya msingi Mama Sara na kurudi shule ya msingi wasso nao watoto walikimbia kilometa 2.5 kwa kuzunguka uwanja wa shule ya msingi wasso. Mbali na mchezo wa riadha mashindano hayo yalishirikisha mpira wa miguu kati ya loliondo sports club na magereza sports ambapo timu ya loliondo sports illishinda.
Washindi wa mashindano ya riadha walikuwa kama ifuatavyo; kilometa 21 wanaume mshindi wa kwanza alikuwa ni Rayket Gamaya (dakika 66), mshindi wa pili Wilson Ngabasi (dakika 69) na Mshindi wa tatu Yotam Gwandu (dakika 72). Kwa mbio za kilometa 10 wanawake mshindi wa kwanza Pendo Ibrahimu (dakika 61), mshindi wa pili Tiweli Saudi (dakika 63) na Mshindi wa tatu Penina Michael (dakika 67). Kilometa 2.5 kwa watoto mshindi wa kwanza ni Emanual Paul mshindi wa pili ni Monika Taiwap na mshindi wa tatu Brayson Elly. Zawadi mbalimbali zilitolewa kwa washindi zikiwemo fedha, vyeti na mipira.
Akitoa shukrani wakati wa kufunga mashindano haya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya aliwapongeza washindi wote na kuwashukuru watu mbali mbali kwa jinsi walivyojitoa kufanikisha mashindano haya . Pia aliishukuru halmashauri ya wilaya ya ngorongoro, GIZ na mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kwa jinsi walivyochangia kufanikisha mashindano haya na aliwaomba wasisite kutusaidia pale tutakapowahitaji kwani huu ni mwanzo tu wa michezo ambayo tutaendelea kuifanya na kuiimarisha ndani ya halmashauri yetu . Aidha mgeni rasmi aliahidi kuyaenzi mashindano haya na kusema kuwa mwakani mashindano haya yatasajiliwa kitaifa hivyo kushirikisha wachezaji kutoka mikoa mbalimbali na kuyafanya makubwa kuliko yanavyoonekana sasa hivyo akawataka wachezaji wajiandae ili waweze kushindana na wachezaji wengine watakao shiriki.
Naye mwenyekiti wa CCM wilaya aliwashukuru na kuwapongeza waandaaji, wawezeshaji na wachezaji wote kwa ujumla pia aliwaomba waandaaji kama ikiwezekana mashindano haya yawe yanafanyika kwa kata ili kupata wachezaji wengi na bora zaidi.
Hata hivyo Mgeni rasmi alifunga mashindano haya kwa kutoa zawadi zikiwemo fedha taslim na vyeti pamoja na mipira.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.