Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani hufanyika tarehe 8 mwezi Machi kila mwaka. Kwa mwaka 2018 maadhimisho haya kitaifa yamefanyika mkoani Arusha na kwa Wilaya ya Ngorongoro yamefanyika kata ya Oloipiri kijiji cha Orkuyeine.
Mgeni rasmi katika maadhimisho haya alikuwa Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mh. Rashid M. Taka ambapo aliwakilishwa na Afisa Utawala na Utumishi (W) Bw. Emmanuel J. Mhando. Mgeni rasmi aliambatana na baadhi ya viongozi wengine akiwemo Afisa Maendeleo ya Jamii (W) Bi Teresia A.Irafay na Wah. Madiwani ambao ni viongozi wa Umoja wa Wanawake wa CCM- UWT (W)
Maadhimisho haya yalianza kwa mdahalo uliofanyika tarehe 7/03/2018 ambapo wanawake na wanaume walioshiriki walijadili changamoto zinazowakumba katika jamii zao, kama vile usawa wa kijinsia katika kumiliki mifugo, elimu na haki ya kuchagua/kuchaguliwa kuwa kiongozi wa ngazi mbalimbali.
Katika kilele cha Maadhimisho hayo, wanawake wametumia siku hiyo kufanya maonyesho ya bidhaa walizotengeza baada ya kupata mafunzo ya ujasiriamali kutoka Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro na mashirika yasiyo ya kiserikali kama PWC (Pastoral Womens Council), Shirika la Focus on Tanzania Society (FoTS Foundation) – chini ya ufadhili wa kampuni ya Utalii ya Tomson Safaris. Bidhaa zilizoonyeshwa ni asali, shanga, kuku, viatu vya wazi, mikanda na nguo za asili zinazotegenezwa na vikundi mbalimbali vilivyopo kweye kata ya Oloipiri na kata ya Ololosokwan.
Pia burudani mbalimbali zilisherehesha siku hiyo kupitia vikundi mbalimbali vya ujasiriamali.
Baada ya maonyesho hayo risala ilisomwa mbele ya mgeni rasmi ikionyesha shughuli walizozifanya, mafanikio na changamoto.
Mafanikio waliyopata ni pamoja na; kuunda na kupata usajili wa vikundi vya ujasiriamali, VICOBA (Village Community Bank), COCOBA (Community Conservation Bank). Kuundwa kwa jukwaa la wanawake wilaya ya Ngorongororo. Changamoto wanazopata ni uhaba wa soko, ubovu wa miundombinu na ukosefu mtaji.
Sherehe hizo zilihitimishwa na hotuba ambapo Mgeni rasmi alielezea namna wilaya ilivyojipanga kuendelea kutatua changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo kama vile kuharakisha utoaji wa mikopo, kuongeza kiwango cha utoaji wa elimu ya ujasiriamali ili kuweza kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa bidhaa zenye kumudu ushindani wa soko la kimataifa na mpango wa serikali kuelekea uchumi wa viwanda. Mgeni rasmi pia alitoa wito kwa wanaume na wadau wa maendeleo kuendelea kuwasaidia wanawake katika shughuli zao na kuachana na mila zilizopitwa na wakati zinazomkandamiza mwanamke.
Aidha Afisa Maendeleo ya Jamii (W) alitoa shukrani zake za pekee kwa mgeni rasmi kwa kumwakilisha Mh. Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, aliwashukuru watu wote wa kata ya Oloipiri kwa kufanya maandalizi na mapokezi makubwa, hasa viongozi wa kata- Mh Diwani Wilium Alais, na wenyeviti wa vijiji vya Orkuyaine, Sukenya na Oloipiri pamoja na watendaji wote wa kata na vijiji. Pia aliwashukuru Maafisa Maendeleo ya Jamii kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa pamoja na ushirikiano wanaounesha katika kazi. Pia aliwashukuru wageni wote kwa kuhudhuria kwa wingi maadhimisho hayo na kuahidi kuwa mwisho wa maadhimisho ndio mwanzo wa maandalizi ya maadhimisho mengine na shughuli zingine za uwezeshaji jamii.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.