Madiwani watano waliojiuzulu kutoka CHADEMA na kujiunga na chama cha mapinduzi (CCM) hatimaye wameapishwa rasmi tarehe 04/09/2018 katika ukumbi wa halmashauri.Hayo yalijiri wakati wa baraza la kawaida la madiwani katika ukumbi wa Halmashuri ya Wilaya ya Ngorongoro. Madiwani hao ni,Joseph Kerei seuri(Pinyinyi), Daniel A. Orkeri (Ngorongoro),sokoine Moir(Alaitole),Boniface M. kanjwel (soitsambu) na Lazaro s. saitoti(ngoile).
Aidha katika baraza hilo Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ndugu Rashid Mfaume Taka alipata nafasi ya kuhutubia baraza la madiwani ambapo katika hotuba yake alisisitiza zaidi juu ya ukusanyaji wa mapato katika halmashauri kwani tumeanza mwaka wa fedha hivyo tunatakiwa kuanza kwa kasi kubwa. Akitolea mfano chanzo cha uuzaji wa viwanja mheshimiwa mkuu wa wilaya alishauri kuwa viwanja vitangazwe na ramani zibandikwe katika mbao za matangazo ili wateja wachague viwanja ndipo waje walipie ada ya maombi pamoja na gharama yote ya kiwanja au walipie kidogo kidogo isipokuwa wasivuke mwaka wa fedha husika. Hii italeta uwazi na itaondoa utaratibu unaotumika sasa ambapo mteja hulipia ada ya maombi na akipata kiwanja anaweza kukaa nacho bila kukilipia kwa muda mrefu. Aliwataka watu wa idara ya ardhi waendelee kupima viwanja na waviuze vyote mwaka huu na kwa vile ambavyo havijalipiwa japo vilishagawanywa vitangazwe upya na viuzwe.
Mheshimiwa mkuu wa wilaya alisisitiza kuwa halmashauri iongeze jitihada katika lango la ngarasero na nyumba za kulala wageni ndani ya hifadhi ya ngorongoro ili kukusanya mapato ya kutosha kwani vyanzo hivi vina viashiria vingi vya upotevu wa mapato. Aidha aliwataka wataalam watumie mfumo wa kusajili wageni wanaolala katika hoteli za kitalii (lodge) unaotumiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na hifadhi ya Taifa ya Serengeti ili kupata idadi kamili ya wageni na kuongeza mapato.
Kwa upande wa elimu mkuu wa wilaya alisisitiza juu ya umaliziaji wa miradi viporo hasa ya ujenzi wa madarasa ili halmashauri iweze kujiandaa kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha tano kwa mwaka 2019.
Mheshimiwa mkuu wa wilaya alieleza kuwa mwenge wa uhuru kwa mwaka huu utapita katika maeneo ya Tarafa ya Ngorongoro hivyo waheshimiwa madiwani washiriki katika mbio za mwenge na kuhamisisha wananchi washiriki kwa wingi.
Katika hatua nyingine baraza lilijigeuza kama kamati na kujadili ripoti ya uchunguzi juu ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali katika miradi ya ujenzi ya kituo cha afya sakala na shule za sekondari za Digodigo, Sale, Nainokanoka na Loliondo na kasha kupendekeza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa watumishi waliohusika katika michakato hiyo.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.