Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro ilifanya mafunzo ya awali kwa watendaji wa vijiji walioajiriwa mwezi Novemba mwaka 2017 yaliyolenga kuwajengea uwezo katika kazi yao. Mafunzo hayo yalifanyikia katika ukumbi wa halmashauri na yalifunguliwa na kaimu mkurugenzi ndugu Emmanuel A. Sukums.
Katika mafunzo hayo kaimu mkurugenzi aliwaasa waajiriwa wapya wawe makini na wasijiingize kwenye siasa badala yake wakafanye kazi za serikali bila upendeleo wakijua kabisa kuwa wanatekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Aidha aliwaambia kuwa kuajiriwa kwao kumetokana na sifa zao na hategemei wamwangushe hivyo wakawe mawakala wema wa serikali huko vijiijni na watoe taarifa kwa wakati pale linapojitokeza jambo lolote kwani wao ni walinzi wa amani katika maeneo hayo.
Pia kaimu mkurugenzi aliwaeleza kuwa mazingira yao ya kazi yana changamoto hivyo wakafanye kazi kwa bidii na kujituma kwani vijiji vyetu vingi vipo mbali na makao makuu ya wilaya. Aliwataka watumishi hao wakawe na mahusiano mema na wananchi na viongozi watakaowakuta na waepuke kuwa vyanzo vya migogoro na kutumia madaraka yao vibaya.
Naye afisa utumishi aliwafafanulia watumishi hao juu ya sheria na taratibu za kazi hasa masuala ya kinidhamu. Pia aliwaeleza kuwa watendaji wa vijiji wanawajibika kwa watendaji wa kata na wote wapo chini ya idara ya utawala hivyo wawe tayari kupokea maelekezo kutoka kwao .
Baada ya ufafanuzi wa afisa utumishi, Mwanasheria wa halmashauri aliwaapisha watendaji hao wapya kisha akawaeleza kuwa wao ni walinzi wa amani hivyo wakadumishe amani badala ya kuwa vyanzo vya vurugu na wakumbuke kuwa wakitenda makosa watahukumiwa wao. Aliwaeleza kuwa watendaji wa vijiji wana mamlaka ya kumweka mhalifu ndani kwa masaa kumi na mbili tu kwa mujibu wa sheria na sii vinginevyo ila akawatahadharisha wasiitumie mamlaka hiyo vibaya.
Semina hiyo pia ilihusisha idara nyingine kama Mipango, Maendeleo ya jamii na Fedha ambapo kila idara ilielezea kwa kina jinsi ya kujaza nyaraka mbalimbali katika ofisi zao huko vijijini.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.