Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa zimeendelea katika Mkoa wa Arusha ambapo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Mashaka Gambo aliupokea Mwenge huo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Daktari Charles Mlingwa. Mwenge huo unataradiwa kupitia miradi mbalimbali yenye thamani ya Takriban Zaidi ya Tsh. Bilion 17. Makabidhiano hayo yamefanyika katika kijiji cha Ololosokwan kata ya Ololosokwan na mwenge huu unatarajiwa kukimbizwa katika Halmashauri zote saba kwa muda wa siku saba. Katika mapokezi hayo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa alisema kuwa Mkoa wa Arusha umejipanga vyema kuhakikisha kuwa kaulimbiu ya Mwaka huu inatekelezwa kwa vitendo na kwa kuanzia ameunda kamati maalum ya kufuatilia viwanda inayoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha na kuweka mkakati wa kuhakikisha kuwa viwanda vyote vya zamani vinafufuliwa upya ili viweze kutoa ajira kwa wananchi.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka Huu Amour Hamad Amour aliwataka wananchi wanaozungunga Hifadhi kulinda rasilimali zilizopo ikiwepo wanyamaapori na kusaidia Serikali kupambana na majangili na kusema kuwa “tusiwe teyari kuona Tembo anauliwa kwa ajili ya kupata meno ya tembo, tusiwe teyari kuona Chui anauliwa kwa ajili ya kupata ngozi”
Akipokea mwenge huo wa uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mheshimiwa Rashid Mfaume Taka amesema ni faraja na heshima kubwa kwa Wilaya kushiriki katika kukimbiza mwenge huo wa Uhuru.
Akisoma Risala ya Utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Daktari John Pombe Magufuli, Mheshimiwa Mkuu wa wilaya alisema Ujumbe wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu unaosema “Shiriki kukuza Uchumi wa Viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu”. Sote tunatambua kuwa viwanda ni chachu ya maendeleo ya Taifa lolote lile hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha viwanda vinajengwa ndani ya Wilaya kwa ajili ya ustawi wa jamii yetu. Katika kufanikisha azma hii ya Serikali Wilaya imekuwa mstari wa Mbele katika kuhamasisha wadau wa maendeleo kuwekeza katika viwanda vya kusindika mazao hasa mazao ya Mifugo kwani Wilaya yetu ni ya Wafugaji. Pia tumekuwa na mipango mahususi kuhakikisha vijana wanajiunga katika vikundi ili kuunganisha nguvu na kuanzisha viwanda vidogo vidogo.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya alisema suala la ujenzi wa viwanda ni uwekezaji unaohitaji mikakati mahususi. Kwa kulitambua hili Wilaya ya Ngorongoro imetenga eneo lenye ukubwa wa hekari 122 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vikubwa na vidogo. Eneo hili limekwisha pimwa na utaratibu wa kupata hati miliki upo katika hatua za mwisho. Eneo hili lipo katika mji mdogo wa Wasso “Kitalu E” umbali wa Kilomita moja (1) kutoka Wasso mjini. Eneo hili linafikika kwani lipo pembezoni mwa barabara kuu ya Loliondo–Arusha.
Aidha tenda ya kusambaza maji katika eneo lote la kitalu E ikiwemo eneo la viwanda imetangazwa na Mkandarasi amekwisha patikana na kazi itaanza muda wowote kuanzia sasa. Kwa upande wa miundombinu ya umeme, umeme upo umbali wa mita 700 tu kutoka katika eneo hili.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya alisema kuwa Wanangorongoro tunaamini kuwa Wanawake na Vijana wakishiriki au kushirikishwa katika nyanja zote za kiuchumi, kisiasa na kijamii Wilaya yetu itapiga hatua kubwa kimaendeleo. Uwezeshaji wa Wanawake na vijana ni suala tunalolipa kipaumbele sana. Kwa sasa Wilaya yetu ina Viwanda vidogo vidogo vitano (5) vinavyo simamiwa na kuendeshwa na Wanawake na vijana. Viwanda hivi vimekuwa na manufaa makubwa kwao wenyewe, familia zao na jamii kwa ujumla.
Suala la Rushwa Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya alisema, Rushwa ni tatizo kubwa na la muda mrefu katika nchi yetu. Ni kikwazo katika mgawanyo wa matumizi ya rasilimali zilizopo katika kutekeleza shughuli muhimu za kuondoa umaskini, njaa na kuwepo maendeleo endelevu. Suala la rushwa limekuwa tatizo sugu lililoenea katika sekta nyingi ndani na nje ya Wilaya yetu. Wajibu wa viongozi wa ngazi zote ndani ya Wilaya umekuwa ni kuwaelimisha wananchi haki zao na kauli mbiu yetu ni “Palipo na rushwa hakuna maendeleo’’ inayokwenda sambamba na kauli ya kitaifa inayotutaka “Tuungane kwa pamoja katika mapambano dhidi ya Rushwa kwa maendeleo, amani na usalama wa Taifa letu.”
Viongozi wa Wilaya kila wakikutana na wananchi wamekuwa wakitoa elimu juu ya madhara ya rushwa katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Katika kipindi cha kuanzia Januari 2016 hadi Desemba 2016 Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ngorongoro imeendelea na jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa. Jumla ya taarifa 48 za vitendo vya rushwa zilipokelewa na kuchunguzwa, kesi 4 zilifikishwa mahakamani. Aidha, katika kipindi hiki TAKUKURU Wilaya imeendesha semina na mikutano ya hadhara kwa wananchi na viongozi wa vijiji kwa lengo la kuhamasisha ushiriki wa jamii katika Mapambano dhidi ya rushwa. Vile vile clubs mbalimbali za wanafunzi zimeanzishwa hasa katika shule za sekondari kwa lengo la kuongeza wigo wa uelewa na mapambano dhidi ya rushwa.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya alisema, Ugonjwa wa UKIMWI bado ni tatizo kubwa katika Taifa letu. Sisi Wanangorongoro tumelifanya suala hili kuwa agenda ya kudumu katika vikao na mikutano yote ya wananchi kwa kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI na kuhamasisha jamii juu ya upimaji wa hiari kupitia vituo vyote vya kutolea huduma za afya (PITC) na kufanya kwa lazima upimaji wa VVU kwa mama wajawazito na wenza wao wakati wa kuhudhuria kliniki ili kumkinga mtoto wakati mama anajifungua (PMTCT). Tangu ugonjwa huu ugundulike nchini mwaka 1983, Watanzania wengi wamepoteza maisha yao. Vijana ndiyo wamekuwa wahanga wakubwa wa janga hili na kwa kutambua hilo Mbio za mwenge mwaka huu zimebeba ujumbe wenye kauli mbiu “Tanzania bila maambukizi mapya, Unyanyapaa na vifo vitokanavyo na UKIMWI; inawezekana ifikapo mwaka 2030”
Sote tunatambua kuwa Taifa linaendelea kupoteza nguvu kazi muhimu kila kukicha na ni ukweli usiopingika kuwa sisi sote tumeguswa kwa njia moja au nyingine na athari zinazotokana na ugonjwa huu. Hii inadhoofisha malengo ya kutokomeza umasikini na nguvu kazi ambayo ingeshiriki kukuza Uchumi wa Viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu.
Katika Wilaya ya Ngorongoro, kwa kipindi cha Julai 2016 hadi Juni 2017 jumla ya watu 20,220 walipimwa afya zao kwa hiari, kati yao wanawake ni 11,063 na wanaume ni 9,157 na waliokutwa na maambukizi mapya ya VVU walikuwa 143 ambapo wanawake ni 94 na wanaume ni 49 na wote wanaendelea kupata huduma za afya.
Mheshimiwa Mkuu wa wilaya alisema kiwango cha maambukizi mapya ya VVU katika Wilaya ya Ngorongoro kimepungua kutoka asilimia 1.7 Julai 2016 hadi asilimia 1 Juni 2017 ukilinganisha na 3.1% ya Mkoa na 5.1% ya Kitaifa. Hii ni kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na wataalamu wa afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kupambana na janga hili. Upo mkakati wa kupambana na maambukizi mapya ya VVU kupitia kamati za kudhibiti UKIMWI kuanzia ngazi ya Kitongoji, Kijiji, Kata hadi Wilaya. Aidha kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tumeendelea kuhamasisha wanawake wajawazito kufika Kliniki na wenza wao, ili kupata ushauri nasaha na upimaji wa hiari na pia kusisitiza matumizi ya kondomu na kupiga vita mila potofu hasa ukeketaji ambao huchangia kwa kiasi fulani kuongeza maambukizi ya VVU. Pia tunaendelea kuhamasisha suala la upimaji wa hiari kwa watu wote ili tuweze kujitambua na kuchukua tahadhari kama tunavyoshauriwa na wataalam wetu, hata leo hii wataalamu wetu wa afya wapo katika eneo hili la mkesha kutoa huduma ya upimaji wa hiari, hivyo wote mnakaribishwa kupima ili kujua hali ya afya zenu.
Katika kupambana dhidi ya malaria Mheshimiwa Mkuu wa wilaya alisema, Katika Wilaya ya Ngorongoro malaria ni miongoni mwa magonjwa yanayo athiri idadi kubwa ya watu. Kundi la watu wanaoathirika zaidi ni watoto wadogo, wanawake wajawazito pamoja na watu ambao kinga yao ya asili ya kupambana na malaria imepungua. Matukio ya hatari zaidi hutokea kwa watu ambao hawajawahi kuugua malaria kwani miili yao haina kinga thabiti ya kupambana na malaria.
Katika Wilaya ya Ngorongoro kumefanyika jitihada mbalimbali katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria. Jitihada hizo ni pamoja na kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya vyandarua vyenye dawa ya kuzuia malaria na kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa dawa mseto za malaria, kuhimiza tabia ya kupata matibabu mapema na kuhimiza matumizi ya dawa za kuzuia malaria kwa kina mama wajawazito. Ujumbe wa Mwenge mwaka huu unatutaka “Tushiriki kutokomeza Malaria kabisa kwa manufaa ya jamii.”
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya alisema Matumizi ya dawa za kulevya huambatana na athari nyingi za kiafya, kijamii na kiuchumi. Baadhi ya athari hizo ni kuwepo kwa magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya akili, homa ya Ini, kifua kikuu, VVU/UKIMWI na magonjwa mengine.
Vijana wengi ambao ndio nguvu kazi na muhimili mkuu wa uchumi wa Viwanda katika nchi wanaathirika. Ipo haja ya kuendelea kupambana na hali hii kwa kuunganisha nguvu na rasilimali kutoka kwa wananchi na wadau wote wenye mapenzi mema na nchi yetu.
Ujumbe wa Mwenge wa mwaka huu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya unatutaka “Tuwajali na tuwasikilize watoto na vijana.” Katika kipindi cha mwaka wa 2016/17 Wilaya iliendelea na jitihada za kupambana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya. Katika kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya, Wilaya imeweka mpango wa kupambana na vichochezi na tabia hatarishi kwa jamii kwa kutoa elimu, stadi za kazi za maisha na ujasiliamali. Vile vile tumeendelea kuhamasisha jamii kubadili mtazamo na kushiriki katika jitihada za kukabiliana na utumiaji wa madawa ya kulevya na athari ambatanishi. Upo mkakati wa kuvibadilisha vijiwe vya vijana kuwa vikundi vya wazalishaji mali ikiwa ni pamoja na kuzuia upatikanaji wa madawa ya kulevya kwa kupambana na wasafirishaji na wauzaji.
Tayari Mwenge wa Uhuru umemaliza mbio zake katika Wilaya ya Ngorongoro na miradi sita ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Tsh. 1,738,779,000 imepitiwa na mwenge wa uhuru miradi hiyo ni pamoja na mradi wa kiwanda cha kuchakata mazao ya mifugo Ololosokwan wenye thamani ya Tsh. 466,900,000, mradi binafsi wa kituo cha mafuta- Wasso (karanjai filling station) wenye thamani ya Tsh. 600,000,000, ujenzi wa bweni1, madarasa manne (4) na matutundu 10 ya vyoo katika shule ya sekondari Loliondo wenye thamani ya Tsh. 259,000,000 Mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Bisikene katika kijiji cha digodigo wenye thamani ya Tsh. 92,879,000, mradi wa ujenzi wa nyumba ya waalimu (6 in 1), madarasa manne na matundu kumi ya vyoo katika shule ya sekondari Lake Natron wenye thamani ya Tsh. 301,000,000 na mradi wa vijana wanaojihusisha na shughuli za utalii katika kata ya Engaresero wenye thamani ya Tsh. 19,000,000. Kati ya miradi hiyo, miradi miwili imetembelewa, miradi 2 imezinduliwa na miradi miwili imewekewa jiwe la msingi. Kati ya miradi miwili iliyotembelewa, mradi mmoja wa kikundi cha vijana cha Utalii Engaresero watakabidhiwa hundi ili kuwaongezea mtaji.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.