Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K Mongella amemkabidhi funguo za gari, aina ya Toyota Land Cruser - Ambulance, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro Mhe. Emmanuel Ole Shangay, wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya magari ya Afya, iliyofanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha leo tarehe 05.12.2023.
Akikabidhi Magari hayo, Mkuu huyo wa mkoa, amewasihi viongozi wa ngazi zote, kusimamia utunzaji na matumizi sahihi ya vitendea kazi hivyo, ili viweze kufanya kazi iliyokusudiwa na Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi na sio kinyume na hivyo, huku akiwasisitiza kutambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassani ya kufikisha huduma karibu na wananchi.
"Viongozi mnalo jukumu kubwa la kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki, wafuatilieni watendaji wa Serikali katika maeneo yenu, hakikisheni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi unawanufaisha wananchi, wananchi wanahitaji suluhu ya changamoto zao kupitia sisi, wahakikishieni utendaji wa serikali yao kwa vitendo" Ameweka wazi Mhe. Mongella.
Hata hivyo Mhe. Ole Shangay, ameishukuru serikali kwa kuzingatia umuhimu wa huduma za afya kwa wanachi wa Ngorongoro, ambao baadhi yao, wanaishi kwenye ameneo ambayo hayafikiki kwa wepesi na kusababisha wakati mwingije kushindwa kupata huduma stahiki kwa wakati.
Amesema kuwa, uwepo wa gari la dharura pamoja gari la Kliniki tembezi,mitasaidia utoaji na upatikanaji wa huduma za afya kwa wakati, huku akiamini zitapunguza uwepo wa vifo visivyo vya lazima hususani kwa watoto na wanawake wajawazito ambao wanahitaji huduma za dharura na haraka wakati wote.
"Wapo watu walipoteza maisha Ngorongoro kwa kukosa ama kuchelewa kupata huduma za afya kwa wakati, kulikosababishwa na changamoto ya jiografia ya maeneo yetu, tunaamini uwepo na upatikanaji wa huduma za dharua utapunguza vifo visivyo vya lazima na wananchi wa Ngorongoro wataendela kuiamini serikali yao makini ya awamu ya sita, chini ya Dkt. Samia Suluhu" Ameweka wazi Mbunge huyo wa Ngorongoro
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.