Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na Benk ya maendeleo ya Ujerumani (KFW) imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali Wilaya ya Ngorongoro ikiwemo ujenzi wa Zahanati, Vyumba vya madarasa, Nyumba za Walimu, Nyumba za Wahudumu wa afya pamoja na barabara.
Miradi hiyo imetembelewa na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Kanali. Wilson Sakulo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku nne iliyoanza jumamosi ya tarehe 24 Februari, 2024 mahsusi kwa ajili ya ukaguzi wa miradi yote inayotekelezwa na KFW chini ya usimamizi wa Kampuni ya CDM Smith.
Aidha Mkuu wa Wilaya ametoa rai kwa Wananchi wanufaika wa miradi hiyo kuweka sawa mazingira ya ulinzi wa vifaa vinavyopelekwa saiti na kutunza na mazingira ili yawatunze.
"Tunzeni mazingira na yawekeni katika hali ya usafi, pia hakikisheni vifaa vyote vinavyofika saiti vinakua salama boresheni hali ya ulinzi na yoyote atayehusika na wizi achukuliwe hatua za kisheria" amesema Kanali. Sakulo
Ziara imetembelea miradi yote inayotekelezwa katika Kata ya Samunge ambayo ni nyumba moja ya Walimu itakayohudumia Walimu wawili katika Shule ya Msingi Mageri yenye thamani ya Shilingi milion 171, nyumba moja ya Mganga, Zahanati ya Mgongo, bwalo la chakula lenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 800 lenye thamani ya shilingi milion 684 katika Shule ya Sekondari Samunge, jengo la Wagonjwa wa nje (OPD) katika Zahanati ya Yasimdito kijiji cha Yasimdito.
Ziara hiyo imemalizikia Kata ya Maalon kijiji cha Loswash kukagua ujenzi wa madarasa mawili ambayo yako katika hatua ya umaliziaji kisha barabara ya Maalon hadi Kipambi yenye urefu wa kilomita 14.6 ambayo tayari imekamilika.
Kwa upande wao Wananchi wa Kata ya Samunge na Maalon wametoa Shukrani zao za dhati kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Tunaendelea kumpongeza Rais kwa miradi hii anayotuletea na tunamshukuru sana kwani miradi hii inatija kwetu sisi kama jamii pia tunawashukuru KFW tunaomba waendelee kutufanyia hisani zaidi".
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.