Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Mhe.kanali Wilson Sakulo amewataka waheshimiwa Madiwani kushiriki kikamilifu kusaidia kutatua migogoro yote iliyopo katika maeneo ya kata zao kwani wao wananguvu kubwa na imani ya Wananchi wao.
Ameyasema hayo katika Mkutano wa baraza la Halmashauri kwa robo ya tatu ya mwaka 2024 kilichofanyika leo tarehe 13 Juni 2024 katika ukumbi wa Halmashauri ya Ngorongoro ambapo amechukua nafasi hio kuwapongeza Madiwani wa kata za Oloipiri na Soitsambu ambao wameweka juhudi za makusudi kumaliza mgogoro wa mpaka kati yao kwa kushirikiana na Viongozi wa mila na amewahakikishia wakimaliza ataishauri Sekta ya ardhi Wilaya kupitisha mipaka itakayo kubaliwa.
Mhe. Sakulo amewasihi Waheshimiwa Madiwani kuwahamasisha Wananchi katika kata zao kushiriki kikamilifu katika zoezi la maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura, zoezi ambalo ameeleza mchakato na taratibu zake zitaanza tarehe 1 Julai, 2024 ili kuhakikisha kwamba ifikapo wakati wa kupiga kura watekeleze haki yao ya kikatiba kwa kuchagua Viongozi huku pia akichukua nafasi hio kuipongeza Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro kuongeza makusanyo ya mapato.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Mohamed Bayo amesema katika kipindi cha mwezi Mei Halmashauri imekusanya kiasi cha sh.178,786,931 na kufanya jumla ya makusanyo kuwa shilingi 2,586,714,284, sawa na 83% ya makisio ya kukusanya jumla ya shilingi 3,101,200,000. Pia ametoa rai kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngorongoro kupitia Diviaheni ya Mipango ikutane na Wenyeviti wa kata na vijiji ili kushughulikia vifungu katika mfumo mpya wa manunuzi inayosababisha vijiji kushindwa kutumia fedha zilizopo katika akaunti zao.
Hata hivyo ameguaia suala la njia za ukusanyaji mapato amebainisha kua Ofisi ya Mkurugenzi ndio inayofanya ukusanyaji wa mapato hasa katika minada na sio Vyombo vya Usalama kama inavyopotoshwa kwani kamati ya fedha katika kikao chake cha mwisho kilichoketi mwezi wa nne kiliridhia kikosi kazi kilichoundwa kikihusisha Kamati ya Usalama kiendelee kusaidia wakusanya mapato kwa kufuatilia kwa karibu upotevu wa mapato hasa katika minada.
Pia, kikao hicho kimepokea na kujadili taarifa za kamati za kudumu za Halmashauri ambazo ni kamati ya kudhibiti UKIMWI,Elimu na Huduma za kijamii pamoja na Kamati ya Fedha. Katika taarifa ya Kamati ya kudhibiti UKIMWI imeeleza kua katika kipindi cha januari hadi Machi waliopima kwa hiari hali ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI wilayani hapa ni watu 4,825 ambapo kutokana na takwimu hizo kiwango cha maambukizi ni asilimia 0.8% ikilinganishwa na 1.9 % ya Mkoa wa Arusha na 4.7% ya kitaifa huku jitihada za kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya Virusi Vya ukimwi na UKIMWI na umuhimu wa upimaji kwa hiari na kuanza matumizi ya dawa za kufubaza Virusi vya ukimwi zikiendelea kufanyika
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.