MKUU WA MKOA WA ARUSHA AZUNGUMZA NA WANANCHI KIJIJI CHA NANI:
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. John VK Mongella amewatembelea na kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Nani kata ya Enguserosambu Wilaya ya Ngongoro, kisha kuzungumza nao katika mkutano wa hadhara.
Wakati akizungumza na Wananchi hao amezitaka Taasisi zinazoshughulia huduma ya miundo mbinu ya kijamii ikiwemo TARURA pamoja na RUWASA, kushughulia changamoto zinazowakumba wananchi. Kero hizo ni pamoja na huduma ya maji safi na salama kwa upande wa RUWASA na miundo mbinu ya barabara kuwekwa vizuri kwa upande wa TARURA.
Aidha Mhe. Mongella amefurahishwa na kitendo cha wananchi wa Nani kushirikiana pamoja kwa kuunga mkono serikali katika shughuli za maendeleo. Pia ametoa shukrani kwa Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo, yote hayo ni kuondoa kero kwa wananchi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
"Rais wetu anafanya juhudi kubwa sana kuondoa kero za wananchi"-amesema Mhe. Mongella
Katika mkutano huo Mhe. mkuu wa mkoa ametoa rai kwa Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi mtendaji wilaya ya Ngorongoro kusimamia miradi yote inayoendelea katika kijiji cha Nani kujengwa katika ubora unaotakiwa.
Katika Hadhara hiyo Mhe John VK Mongella ametoa ahadi ya kurudi tena kutembelea wananchi na Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za wananchi kwa kutoa fedha kwaajili kukamilisha miradi yote ya maendeleo inayoendelea kwa sasa na kuleta miradi mingine.
Hata hivyo amewambia wananchi wa kijiji cha Nani kuwa vitambulisho vya Taifa (NIDA) vimekwisha anza kutolewa kwa wananchi wote ambao waliyokuwa wamejiandikisha na baada ya wiki mbili wananchi wote wanaostahili kuwa na vitambulisho watakuwa wamepata vitambulisho vyao. Ufafanuzi huo ametoa wakatia anajibu hoja ya wananchi kuhusu changamoto ya kutokua na vitambulisho vya taifa.
Kwa upande wa wananchi Mhe.Olemilia diwani kata ya Enguserosambu amesema kuwa Wananchi wa Kijiji cha Nani na kata ya Enguserosambu kwa ujumla wanatoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan.
"Rais wetu ameendelea kutuletea miundo mbinu yote ya kijamii kama zahanati na shule na hata hali ya usalama sasa ni nzuri ukilinganisha na hapo awali, tunaendelea kumuomba aendelee kutuongezea miradi zaidi". amesema Mhe. Diwani
Ikumbukwe Mhe. Mkuu wa mkoa wa Arusha amekua na ziara ya siku tatu katika Wilaya ya Ngorongoro, na ziara hiyo ilianza tarehe 10 Novemba na inatarajia kumalizika tarehe 12 Novemba 2023.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.