Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro Bw.Murtallah Sadiki Mbillu amemsimamisha kazi Tabibu msaidizi Zahanati ya Misigiyo kupisha uchunguzi kwa tuhuma za Wizi wa dawa na vifaa tiba
Akizungumza ofisini kwake, Bwana Mbillu amesema kuwa amemsimamisha kazi Ndg. Samweli Panga ambaye ni Tabibu Msaidizi kwa kukamatwa na dawa na vifaa vya tiba vyenye thamani ya shilingi 344 ,213.90 akiwa anaviuza katika mnada wa Olbalbal mnamo tarehe 13 Juni 2024.
Pia, Mkurugenzi amesema kuwa mtumishi huyo alikamatwa baada ya kupata taarifa za siri na kuweka mtego ambao ulifanikisha kumkamata akiwa na vifaa vya tiba na dawa ambazo Serikali inatumia gharama kubwa kununua.
Mkurugenzi ametoa onyo kwa Watumishi wote wa Halmashauri ya Ngorongoro kufuata Sheria, taratibu na Kanuni za Utumishi wa Umma na hatosita kumchukulia hatua Mtumishi atakayebainika kuwa na tabia ya wizi na kutojali kazi yake.
Aidha, Mganga mkuu wa Wilaya Daktari Libori Tarimo katika kuelezea suala hilo amesema amelaani kitendo hicho na hatomfumbia macho mhudumu yoyote wa afya atakayeenda kinyume na maadili ya kazi
"dawa za Serikali na vifaa tiba vitumike kwa lengo lilillokusudiwa na Serikali na sii vinginevyo" amesema Dkt. Libori.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.