Mhe. Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameungana na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwashukuru wadau wote pamoja na wananchi waliojitokeza kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwaokoa wahanga wa jengo la ghorofa nne lililoanguka katika Mtaa wa Mchikichi na Manyema uliopo Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Mhe. Majaliwa ametoa shukrani hizo leo alipolitembelea jengo hilo lililoanguka Novemba 16, 2024 kwa lengo la kujiridhisha na zoezi la ukoaji linaloendelea, ambalo linaongozwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi waliojitolea.
“Nawashukuru wadau wote wa sekta binafsi na sekta za umma pamoja na wananchi walioiunga Serikali mkono katika zoezi la kuwaokoa wahanga wa ajali hii kwa kujitolea vifaa mbalimbali, mitambo, magari na wataalam ambao wanashiriki katika zoezi la uokoaji linaloendelea,” Mhe. Majaliwa amesisitiza.
Mhe. Majaliwa amesema, wakati Serikali ikiendelea kujiimarisha katika idara ya maafa na uokozi kuna umuhimu wa kuendelea kushirikiana katika jambo la dhalura kama hili la ghorofa kuanguka kwa ghorofa, kwani jambo hili si la Serikali pekee bali ni la watanzania wote.
“Tunakiri kwamba mchango wa wadau na wananchi ni mkubwa na umesaidia kuokoa wenzetu 84 ambao ni wahanga wa tukio hili na ninawahakikishia watanzania kuwa, zoezi la uokoaji linaendelea mpaka tutakapojiridhisha kwamba wote waliopo ndani ya jengo hili wameokolewa wakiwa hai au tumewapoteza kwa mapenzi ya Mungu,” Mhe. Majaliwa ameeleza.
Sanjali na hilo, Mhe. Majaliwa amewashukuru wafanyabiashara wa Kariakoo kwa utulivu wao wakati huu ambao zoezi la uokoaji likiendelea na amewataka kuendelea kuwa watulivu ili kutoa fursa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kutimiza jukumu la uokoaji wa wahanga ambao bado wapo katika jengo hilo lililoanguka. Ili kuongeza ufanisi katika zoezi la uokoaji, Mhe. Majaliwa amemuelekeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila kufunga barabara ambazo matumizi yake yanaathiri zoezi la ukoaji, lengo likiwa ni kuruhusu mitambo kuingizwa kwa urahisi pamoja na kuwawezesha waokoaji kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi na weledi.
Aidha, amemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kumtafuta mmiliki wa jengo lililoanguka ili aanze kulisaidia jeshi la polisi katika kubaini chanzo cha jengo hilo kuanguka, na kuleta madhara yalipopelekea watu kupokeza uhai, hasara kwa wafanyabiashara na Serikali kuingia gharama.
Mara baada ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kujiridhisha na zoezi la uokoaji katika jengo hilo lililoanguka Karikakoo jijini Dar es Salaa, alielekea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja na kuwaongoza watanzania kuaga miili ya waliofariki kwenye ajali hiyo
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.