Mahakama ya Wilaya Ngorongoro imeadhimisha siku ya sheria kitaifa leo tarehe 3 Februari 2025 kwa ngazi ya Wilaya iliyofanyikia katika ukumbi wa mahakama hiyo, ikiwa kitaifa maadhimisho hayo yamefinyikia Jiji la Dodoma.
Mgeni rasmi katika siku ya sheria ngazi ya Wilaya ni mheshimiwa hakimu mkazi mfawidhi mahakama ya Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Saida Steven na mgeni maalumu ni mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Kanali Wilson Sakulo.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kilele Cha wiki ya sheria Mhe. Kanali Sakulo ameipongeza mahakama ya Wilaya kwa kuendesha shughuli wiki nzima kwa kutoa Elimu ya masuala ya kisheria na kutatua changamoto mbalimbali za kisheria kwa wananchi.
"Rai yangu kwenu ni kuendelea kutoa elimu zaidi mambo ya kisheria hata mara baada ya kumaliza kwa wiki ya sheria ili kuendelea kutatua changamoto nyingi za kisheria katika jamii zetu"-Mhe. Kanali Sakulo.
Mgeni rasmi wakati akihutubia katika maadhimisho hayo ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau wote wa mahakama, viongozi, Wananchi kwa ushirikiano wa kutosha wanaoendelea kupitia mahakama pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuanzia taasisi ya Mama Samia Legal Aid Campaign kama njia ya kuwafikia Wananchi wenye changamoto za kisheria mpaka ngazi Wilaya na maeneo yake.
Aidha amesema kuwa mahakama kwa nafasi yake katika kuadhimisha wiki ya sheria na kilele cha siku ya sheria kitaifa imeendelea kutoa elimu ya sheria sehemu mbalimbali ikiwemo mashuleni, kwenye Vituo vya redio, vyuoni, magereza na maeneo mengine ya wazi ili kuwafikia Wananchi wengi zaidi.
"Mahakama imewafikia Wananchi mbalimbali kuwapa elimu ya sheria, pia mahakama imefanya maboresho makubwa katika utoaji haki na tumeweza kufanya maboresho yanayoonekana kwa kuzingatia dira ya Taifa ikiwemo kujenga majengo mapya ya mahakama, matumizi ya mifumo ya usikilizaji wa mashauri kwa njia mtandao, pamoja utunzaji na upatikanaji wa nyaraka za mahakama" amesema Mhe. Saida.
Wiki ya sheria imeenda sambamba na kaulimbiu unayosema "TANZANIA YA 2050: NAFASI YA TAASISI ZINAZOSIMAMIA HAKI MADAI KATIKA KUFIKIA MALENGO MAKUU YA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO".
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.