Kituo cha Afya Sale kilichopo kata ya Sale kimepokea Vifaa vipya vya tiba kwaajili ya upasuaji kutoka Serikali kuu, ili kufanikisha huduma ya upasuaji itakayoanza kutolewa katika kituo hicho hivi karibuni ambapo Kituo hicho kinatarajiwa kuhudumia Wananchi kutoka Kata Malambo, Pinyinyi, Oldonyosambu na Sale yenyewe.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Kanali Wilson Sakulo ameambatana na Wataalamu kutoka Halmshauri mpaka Kituo hicho cha Afya kwa ajili ya kukabidhi vifaa hivyo kisha kufanya Mkutano wa hadhara na Wananchi wa Sale ili kusikiliza na kutatua kero zao.
Aidha Mhe. Sakulo amewaeleza Wananchi mazuri yanayo fanywa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan hasa katika kuleta miradi ya maendeleo kwa kuboresha miundo mbinu ya kijamii katika kata ya Sale kuanzia sekta ya Elimu, Maji pamoja na Afya hususani vifaa vya tiba ya upasuaji ambavyo vitakwenda kutumika kusaidia maisha ya watu
"Mhe. Rais katoa milioni 370 za kitanzania kununua vifaa hivi na kuelekeza kuletwa katika Kituo hiki cha Afya, tumpongeze Rais wetu anafanya kazi kubwa kuhakikisha tunakua kimaendeleo" amesema Kanali. Wilson Sakulo
Hata hivyo wakati wa Mkutano huo Mhe. Mkuu wa Wilaya ameongezea kwa kutoa rai kwa Uongozi wa Kata na Kijjiji kuboresha na kudumisha ulinzi wa eneo zima la kituo cha Afya
"Kuanzia leo nataka ulinzi uimarishwe hapa, maana tunatakiwa kuvilinda vifaa hivi kwani vinathamani kubwa na vina tija kwetu sote" ameongeza Kanali. Sakulo
Akizungumza wakati wa Mkutano huo Diwani wa Kata ya Sale Mhe. Hamza Masedo amesema Serikali ya awamu ya sita inajitoa sana katika kuboresha miradi ya maendeleo na katika kujali afya za Watanzania.
"Mama ameamua Sale vipelekwe vifaa vya kusaidia Wananchi wangu, mfano wazazi kujifungua, upasuaji, dawa za kutosha zinapatikana. Vifaa tulivyoletewa vinapatikana hata katika Hospitali kubwa ikiwemo Hospitali yetu ya Wilaya ya Ngorongoro"-Mhe. Masedo
Pia Mhe. Masedo amemueleza Mkuu wa Wilaya kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu Serikali ya Mama Samia imetekeleza miradi ya maendeleo katika nyanja zote zenye thamani ya shilingi bilion 2.7.
Kwa upande wake Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ngorongoro (OCD) Alphonce Bandia ametoa rai kwa Wananchi wa Sale wanakua mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanakwenda na wale watoro wanafika shuleni kabla hatua kali za kisheria hazijaanza kuchukuliwa.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.