NGORONGORO, 18 Agosti,2021.
Na Mwaandishi wetu.
Shirika la Mimutie Women Organization laendesha warsha ya kuimarisha mahusiano ya wadau wa mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake wilayani Ngorongoro .
Akizungumza hii leo katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya Mh.Mwl Raymond Mwangwala amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Bi.Rose Njilo kwa kuendelea kuihamasisha jamii ,kuhusu ukatili wa kijinsia na athari zake dhidi ya watoto na wanawake katika jamii hususan kwa jamii za kifugaji kupitia shirika lake na kuahidi kuwa serikali watatoa ushirikiano katika mapambano hayo.
Aidha Mh.Mwangwala ameisihi jamii kubadilika na kuachana na mila potofu zinazoweza kuhatarisha maisha ya watu hasa kwa wanawake na watoto watokao katika jamii hiyo.
Kwa upande wake Bi.Rose amesema kuwa shirika hilo linajishughulisha na utetezi wa haki za watoto na wanawake katika kutokomeza ukatili wa kijinsia zaidi katika jamii za kifugaji ambako imeonekana kuwa kitovu cha ukatili huo kwa baadhi ya watu.
Bi.Rose ameongeza kuwa lengo la warsha hiyo ni kukutanisha na kuwaleta pamoja mabaraza ya wanawake pamoja na viongozi wanawake waliochaguliwa au kuteuliwa na mifumo iliyowekwa wilayani Ngorongoro kama vile Polisi dawati,Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa -TAKUKURU- na wadau wengine ambao wanashirikiana katika kutokomeza vitendo hivyo na kujenga mtandao utakao wezesha upatikanaji wa haki wa vikundi hivyo viwili.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti diwani wa viti maalumu Mh.Juliana Samawa ambaye amesema kuwa ukatili wa kijinsia ni mgumu na haupendezi katika jamii na kusema yeye angependa kuona jamii inapewa elimu, ili waweze kufahamu kuwa vitendo hivyo ni hatari ndani ya jamii hivyo ni vyema wanawake na watoto wakapata haki zao za msingi.
Warsha hiyo ya siku moja imehudhuriwa pia na wadau wengine ambao ni wakuu wa idara mbalimabli kutoka halmashauri,dawati la jinsia wilaya,na baadhi ya wawakilishi wa wananchi kutoka kata tofauti.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.