Wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro wahamasishwa kuchangamkia fursa za kukuza uchumi kwa kubadili utamaduni wa asili kuwa utalii wa utamaduni na kuvutia wageni wengi.
Yamesemwa hayo na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Muheshimiwa Mfaume Taka alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya tamasha la utalii wa utamaduni lijulikanalo kama tamasha la utalii wa utamaduni wa Masai Ngorongoro.
Mfaume Taka amesema, wilaya ilikuwa na mpango huo kwa muda mrefu sana baada ya kuona kuwa kuna haja sasa wananchi wa wilaya hiyo kunufaika na mila na desturi zao ambazo zimetunzwa kwa muda mrefu sana na kuzibadili na kuweza kuingiza kipato kwa wananchi na wilaya kwa ujumla.
Amesema, wilaya yake ipo tayari kushirikiana na kila mdau ambae atakuwa tayari kutangaza utamaduni wa makabila yaliyopo humo ili kuuenzi na kuwa kivutio bora zaidi kwa wageni hasa watalii kutoka nchi za nje wanaopenda kuona na kujifunza vitu vya asili.
Akielezea juu ya tamasha hilo Mkurugenzi wa kampuni ya Trace Hills Mgema Mhina,amesema kampuni hiyo kwa kushirikiana na wilaya ya Ngorongoro imeanda tamasha hilo ambalo litajumuisha maonesho ya mila na desturi za makabila yaliyomo katika wilaya hiyo ya Wamasai, Wasonjo,Watindiga na Wamang’ati.
Amesema ,kutakuwa na maonesho ya mavazi ya asili,mitindo ya nywele, mapambo ya asili, michoro ya asili, vyakula ,ngoma za asili za makabila hayo,kampuni za utalii, bidhaa za utamaduni, vinywaji na nyama choma ili watu mbalimbali wakiwemo wageni waweze kujifunza zaidi.
Aidha, amesema malengo ya tamasha hilo ni kukuza utalii na utamaduni wa makabila hayo na kuutambulisha kitaifa na kimataifa, kukuza uchumi kwa wananchi wa Ngorongoro na nchi kwa ujumla na litaweza kutuza mazingira ya hifadhi .
Akisisitiza zaidi Mzee wa Kabila la Kimasai Wiliam Ole Seki, amesema Ngorongoro ndio mahali pekee ambapo mila na desturi za makabila bado zinaenziwa kwa kiasi kikubwa bila kuingila na tamaduni za makabila mengine au nchi nyingine.
Amesema makabila yaliyopo katika wilaya hiyo bado yanafanya kazi kubwa ya kuhakikisha mila na desturi zinaenziwa na mazingira yake ya asili yanatunzwa kizazi hadi kizazi.
Tamasha la utalii wa utamaduni Ngorongoro linatarajiwa kufanyika Septemba 18 hadi 20 katika kiwanja cha Waziri Mkuu Wasso Loliondo na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo watalii.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.