Shule ya Msingi Mairowa iliyopo wilayani Ngorongoro imeendelea kuwa mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa afua za lishe bora kwa wanafunzi. Shule hii ni miongoni mwa taasisi zilizopiga hatua kubwa katika kuhimiza na kuboresha afya ya wanafunzi kupitia ulimaji wa bustani za mboga na matunda kama njia ya kuongeza upatikanaji wa lishe bora shuleni.
Tathmini hiyo imefanyika baada ya Katibu Tawala Hamza H. Hamza Wilaya kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. kufanya ziara ya uhamasishaji katika shule hiyo tarehe 25 Julai 2025. Ziara hiyo iliambatana na Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Libori Tarimo, pamoja na Maafisa Lishe wa Wilaya, kwa lengo la kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa mikakati ya lishe kwa wanafunzi katika mazingira ya shule.
Katika ziara hiyo, Mhe. Hamza alisisitiza kuwa kila shule wilayani Ngorongoro inapaswa kuwa na bustani ya mbogamboga kama njia ya kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe bora. Aidha, alimtaka Mganga Mkuu wa Wilaya kuhakikisha kitengo cha lishe kinasimamia kwa karibu utekelezaji wa mpango huo ili kufanikisha lengo la kuwajengea watoto afya bora ya mwili na akili.
Mwanafunzi Lesiata wa darasa la saba katika shule hiyo alieleza kuwa uwepo wa bustani ya mboga shuleni umeleta manufaa makubwa kwao, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa chakula chenye virutubisho muhimu. “Kupitia bustani hii tumepata maji ya kutosha na tunapata chakula chenye mchanganyiko wa mboga hapa hapa shuleni,” alisema kwa furaha mbele ya viongozi wa Wilaya.
Afisa Lishe wa Wilaya ya Ngorongoro, Bi. Mariamu Ibrahim, alieleza kuwa mbogamboga zina vitamini nyingi ambazo husaidia kuimarisha kinga ya mwili, kuongeza damu, na kupunguza hatari ya maradhi ya mara kwa mara kwa wanafunzi. Aliongeza kuwa lishe bora huongeza uwezo wa watoto kujifunza kwa ufanisi na kuboresha mahudhurio shuleni.
Utekelezaji wa mpango huu wa bustani za lishe mashuleni ni sehemu ya mkakati wa Wilaya ya Ngorongoro wa kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunza kwa afya njema. Halmashauri inaendelea kuhamasisha shule nyingine kuiga mfano wa Shule ya Msingi Mairowa ili kuhakikisha kila mtoto anapata lishe bora katika mazingira ya shule.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.