Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Kituo cha Msaada wa Kisheria Ngorongoro (NGOLAC) yakabidhi magodoro na vifaa kadhaa kwa gereza la Loliondo. Hii ni kama msaada kutoka kwa mashirika haya mawili kwa ajili ya wafungwa na mahabusu wa gereza hilo.
Gereza la Loliondo ni moja ya gereza kongwe na lenye historia kubwa sana. Gereza hili lilijengwa na kuanzishwa mwaka 1922, ikiwa ni gereza la tatu nchini Tanzania (kabla pakijulikana kama Tanganyika kwa mwaka 1922).
Kwa sasa, gereza hilo lina jumla ya wafungwa 80, na mahabusu 21. Mkuu wa gereza, SP George Osindi, aelezea kuwa gereza hilo limejitosheza kwa asilimia 90 kwa upande wa maeneo ya kuhifadhi wafungwa.
Mkuu wa gereza na uongozi mzima wa gereza la Loliondo wameishukuru sana THRDC na NGOLAC kwa msaada huo wa magodoro pamoja na vitu vingine vilivyoletwa na mashirika hayo, na kukiri kuwa walikua na uhitaji mkubwa sana. SP George Osindi atoa wito kwa mashirika mengine kuiga mfano wa mashirika haya kwa wafungwa, kwa maana wana mahitaji mengi sana.
Mratibu Kitaifa wa THRDC, Bw. Onesmo Olengurumwa amepongeza sana uongozi wa gereza la Loliondo kwa hali nzuri na ya usafi kwenye gereza hilo. Mazingira ya gereza hilo pia ni mazuri na rafiki sana kwa wafungwa kupata ujuzi mbalimbali kama vile utunzaji wa bustani, ufundi seremala, ujenzi, nk. Pia aeleza kuwa magodoro na zawadi hizi zimekabidhiwa ikiwa ni moja ya jitihada za kuboresha na kuimarisha haki za binadamu, kupitia misingi ya haki jinai. Na kwa upekee wake, Mratibu atoa wito kwa mashirika na wadau wengine kujitahidi kuimarisha haki jinai nchini kwa njia ya utoaji huduma kwa wafungwa na mahabusu.
Haya yote yamefika Mratibu Kitaifa akiwa katika ziara yake ya kutembelea wanachama wa THRDC kwa kanda ya kaskazini (Manyara, Arusha na Kilimanjaro). Ziara hii ina malengo mbalimbali, ikiwemo sekretariat ya Mtandao kuona ofisi za wanachama wake, kushuhudia kazi wanazozifanya mikoani na wilayani, kufahamu changamoto zinazowakabili na kuzijadili, na kukumbusha majukumu yao kama wanachama.
Mratibu alipata wasaa wa kutembelea tarafa ya Ngorongoro kuona utekelezaji wa ahadi ya Mh. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya kurudisha huduma kwa jamii, pamoja na vijiji vilivyofutiwa shughuli za uchaguzi. Mratibu alipata nafasi ya kuongea na wananchi wenyewe, viongozi wa wananchi, viongozi wa Halmashauri na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuhusu suala hili la tarafa ya Ngorongoro na kurudishwa kwa zoezi la uchaguzi.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.