Sensa ya watu na makazi ni muhimu katika kupata takwimu za Msingi zifuatazo.
Takwimu kuhusu Umri; zitaonesha uwiano kati ya watoto waliofikia umri wa kwenda shule na wale ambao hawajafika umri huo, watu wanaojishughulisha na shughuli za uzalishaji mali na wale wanaotoa huduma,nk.
Takwimu za Elimu; Zitaonesha uwiano kati ya wanaojua kusoma na Wasiojua kusoma,wenye viwango mbalimbali vya elimu, watoto wanaosoma shule ikilinganishwa na wale wasiosoma ambao walipaswa kuwa shule
Takwimu za kiuchumi; Zitaonesha uwiano wa watu wanaofanya kazi na aina ya kazi, takwimu hizi zitasaidia katika kupanga mipango ya maendeleo inayolenga kukuza ujuzi wa wafanyakazi na utoaji wa ajira kwa Vijana
Takwimu za idadi ya Watoto; Zitaonesha hali ya uzazi na Vifo vya watoto kitaifa, Takwimu hizi zitaonesha kiwango cha ongezeko la watu na pia zitawezesha kufanya makadirio ya idadi ya watu katika miaka ijayo kwa nchi nzima,kimkoa,kiwilaya na hata katika ngazi ya chini ya kiutawala
Takwimu za sensa zitasaidia katika kutathmini huduma za afya ya mama na mtoto. Hili ni muhimu katika kuweka mikakati ya kupambana na vifo vinavyosababishwa na matatizo ya uzazi
Watu wanaostahili kuhesabiwa wakati wa sensa.
Watu wanaostahili kuhesabiwa wakati wa sensa ni wafuatao
Watu wote waliolala katika kaya usiku wa kuamkia siku ya sensa
Wale wote ambao hawakulala katika kaya hiyo usiku wa kuamkia siku ya sensa lakini walikuwa wamekwenda shambani kulima,Kuvua,Kuwinda,machungani au wako katika kazi za usiku(mfano, madaktari,askari,walinzi,wahudumu wa hoteli,wauguzi nk.) na waliolala katika msiba jirani na kaya Zao.
Wageni na watumishi waliolala katika kaya hiyo usiku wa kuamkia siku ya sensa
Watu walio katika kaya za Jumuiya, kama vile hoteli, magereza,bweni,Hospitali nk. Na walilala katika kaya hizo za jumuiya usiku wa kuamkia siku ya sensa
Watu wote wasio na makazi maalum au wale wanao hamahama,ambao walilala nchini usiku wa kuamkia siku ya sensa
Watu wote ambao walilala nchini usiku wa kuamkia siku ya sensa, lakini kutokana na shughuli zao hulazimika kuvuka mpaka wa nchi kila siku kwenda nchi nyingine
Watu wote ambao sio raia lakini wanaishi nchini na walilala nchini usiku wa kuamkia siku ya sensa
Wasafiri ambao wako kwenye meli zikiwemo za kijeshi,magari,ndege,garimoshink. Ambao walikuwa nchini usiku wa kuamkia siku ya sensa bila kujali vyombo hivyo ni vya hapa nchini ama ni nje ya nchi
Watu wote waliofariki baada ya saa 6 usiku wa kuamkia siku ya sensa
Watoto wote waliozaliwa kabla ya saa 6 usiku wa kuamkia siku ya sensa na
Mabalozi wa nchi za nje watakaolala nchini usiku wa kuamkia siku ya sensa
Watu wasiostahili kuhesabiwa wakati wa Sensa
Watoto waliozaliwa baada ya saa 6 usiku wa kuamkia siku ya sensa.
Watu wote waliofariki kabla ya saa 6 usiku wa kuamkia siku ya Sensa.
Watu ambao wanaishi nje ya nchi lakini kutokana na shughuli za kikazi huvuka mpaka na kuingia nchini kufanya kazi kila siku na kila jioni hurudi nchini kwao.
Watanzania wote ambao wako nchi za nje na ambao hawakulala nchini usiku wa kuamkia siku ya sensa.