Mji mdogo wa Loliondo pamoja na vijiji jirani, ikiwemo Lopoluni na Oldonyowasi, vinakaribia kushuhudia maboresho makubwa ya upatikanaji wa maji safi kufuatia ujenzi wa tenki la maji lenye ujazo wa lita 300,000 na mtandao wa mabomba wenye urefu wa zaidi ya kilomita 30. Mradi huu umefikia hatua muhimu ya maendeleo na unatarajiwa kuboresha upatikanaji wa maji safi kwa zaidi ya asilimia 85 kwa wakazi wa maeneo haya.
Kwa mujibu wa Mhandisi Gerald Andrew, Meneja wa Wakala wa Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Ngorongoro, mradi huo umefikia asilimia 90 ya utekelezaji. Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi huo, Mhandisi Gerald alisisitiza kuwa mradi huu unalenga kutatua changamoto za muda mrefu za upungufu wa maji safi, hali ambayo kwa miaka mingi imeathiri maisha ya wakazi wa Loliondo na vijiji jirani.
Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano wa serikali ya awamu ya sita na wadau wa maendeleo kutoka Falme za Kiarabu na unatarajiwa kuanza kutumika rasmi mara baada ya kukamilika kwake. Kukamilika kwa mradi huu kunatarajiwa kuleta ahueni kubwa kwa wananchi kwa kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama karibu na makazi yao.
Wananchi wa Loliondo na vijiji jirani watakua wanufaika na huduma za maji safi zitakazosaidia kuboresha maisha yao ya kila siku. Hii ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha huduma muhimu za kijamii zinawafikia wananchi.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.